WAZIRI JAFO ASISITIZA KUSHINDANA KWA HAKI
Na Nora Damian, The Page
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo amewataka wafanyabiashara nchini kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia haki na usawa bila kukwazana ili kukuza sekta hiyo na uchumi wa nchi.
Akizungumza Desemba 5,2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani amesema Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Biashara ya mwaka 2003 na Sheria ya Ushindani namba 8 ya mwaka 2003 ambazo zote kwa pamoja zinalenga kuwawezesha wadau katika sekta hiyo kushindana kwa usawa bila kukwazana.
Aidha amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwasilisha maeneo yote ya kisheria na kikanuni yanayokwamisha wafanyabiashara na kusababisha kushindwa kushiriki vizuri katika ushindani.
“Tunapoadhimisha siku hii lazima tujitathmini kwamba nini tunapaswa kukifanya kuhakikisha tunazidi kusonga mbele, lengo kubwa watu washindane kwa haki, usawa bila mmoja kumnyong’onyesha mwenzake…katika hili naishukuru FCC (Tume ya Ushindani) kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kila wakati,” amesema Dk. Jafo.
Waziri huyo pia amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa FCC kuhakikisha kwamba anaimarisha mifumo ya kushajihisha biashara hasa katika michakato ya maunganiko ya makampuni ili yashughulikiwe haraka kurahisisha uwekezaji na kuongeza ajira.
Dk. Jafo pia amewataka wafanyabiashara nchini kutumia fursa ya masoko mbalimbali likiwemo Soko la Afrika Mashariki, Soko la SADC na Soko Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambalo wanaweza kufanya biashara na nchi zaidi ya 50 kwa kuzalisha bidhaa bora zitakazokidhi ushindani.
Ametolea mfano wa Soko la Marekani (AGOA) ambalo Tanzania imepewa fursa ya kuuza bidhaa zaidi ya 6,500 lakini mauzo yanayofanyika hayaakisi uhalisia wa bidhaa zilizopo kwani inauza wastani wa Dola milioni 85.
“Bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika soko hilo kwa sababu tuna bidhaa nyingi na tuna fursa hii kubwa hivyo, ni lazima tutengeneze bidhaa zenye ubora zinazokidhi ushindani ili tukuze uchumi wetu,” amesema Dk. Jafo.
Amesema maadhimisho hayo yatumike kupeana uelewa wa sheria, sera na kanuni mbalimbali ili kuzalisha bidhaa za ushindani bila kudhuru biashara za watu wengine.
Mwenyekiti wa Bodi ya FCC, Dk. Aggrey Mlimuka, amesema maadhimisho hayo yanaangazia namna sera na sheria za ushindani zinavyotumika katika kupunguza kukosekana kwa usawa katika uchumi.
Amesema lengo ni kuhakikisha sera na sheria zinakuwa katika usawa wa kuleta ushindani katika kuuza, kununua bidhaa na kutoa huduma kwenye soko bila kuwapo na vikwazo.
“FCC imejipanga kutoa huudma bora kwa wateja na wadau kwa kusimamia vyema soko ili kuondoa kukosekana kwa usawa kwa bidhaa zinazoingia sokoni,” amesema Dk. Mlimuka.
Naye Mwenyekiti wa Barala la Ushindani, Jaji Salma Maghimbi, amesema watu wengi bado hawana uelewa wa sera na sheria ya ushindani huku akisisitiza kuwa ushindani ukisimamiwa manufaa huonekana kwenye bei za bidhaa pamoja na huduma bora zinazomnufaisha mlaji.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema wanatumia sera na sheria kuhakikisha fursa za ushiriki katika uwekezaji wa biashara unafanyika vizuri.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Bunge kwa marekebisho ya Sheria ya Ushindani hatua itakayowezesha shughuli zao kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema; ‘Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa katika Uchumi’.


