DMI WAJIVUNIA ONGEZEKO LA WANAFUNZI WAKING'ARA KIMATAIFA

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, akizungumza wakati wa kongamano la tatu la wahitimu wa chuo hicho.


Na Nora Damian, The Page

Kuwepo kwa fursa mbalimbali katika sekta ya bahari kumechangia ongezeko la wanafunzi katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kutoka 1500 hadi kufikia 5100 mwaka huu.

Chuo hicho kilichoanza kama kitengo kiliundwa rasmi mwaka 1991 kuwa chuo cha elimu ya juu na kupewa majukumu makubwa matatu ikiwemo kutoa elimu na mafunzo kama vile kozi za ubaharia na nyingine zinazohusiana na hilo.

Akizungumza leo Desemba 4,2024 wakati wa kongamano la tatu la wahitimu wa chuo hicho, Mkuu wa DMI, Profesa Tumaini Gurumo, amesema wamegusa maeneo yote kutokana na uhitaji uliopo wa rasilimali watu wenye weledi ili kupata wataalam kutoka ndani ya nchi.

"Idadi ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, elimu ya bahari inazidi kuenea vijana wanaziona fursa zilizoko katika sekta hii na kuchangamkia.

"Kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati bado hakuna chuo kinachofikia viwango vya DMI," amesema Profesa Gurumo.Aidha amesema wameanzisha kozi 11 za maafisa wa melini ambapo pia wanatoa kozi za shahada ya uzamili, shahada ya kwanza, stashahada na ngazi ya cheti.

Kwa mujibu wa Profesa Gurumo, tangu mwaka 2019 wahitimu 3,829 wamehitimu katika chuo hicho wakiwemo pia wahitimu 15,000 wa kozi fupi za usalama baharini.

Profesa Gurumo amesema chuo hicho kinashirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, kampuni za meli na vyuo ambapo kampuni zimekuwa zikitoa nafasi kwa wanafunzi kwenda kufanya mafunzo ya vitendo melini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Joseph Abdallah Meza, akizungumza wakati wa kongamano la tatu la wahitimu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).

Ametoa mfano wa Kampuni ya Azam ambayo inachukua wanafunzi zaidi ya 200 kila mwaka kwa ajili ya mafunzo ya miezi mitatu.

"Tuna Ushirikiano na Central Corridor ambao wanatoa ufadhili ili kuimarisha sekta ya bahari, tuna ushirikiano na Korea ambao wameanza kutoa ufadhili wa vijana wetu kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo.

"Mwaka jana vijana wanne walikwenda na mwaka huu watano na vijana wetu walishika nafasi ya kwanza kati ya nchi 13 zilizoshiriki mafunzo hayo...tunatarajia kutengeneza maofisa mahiri kupitia ushirikiano huu," amesema.

Amesema pia wanaangalia namna ya kuweza kuwafikia wadau wengi zaidi na tayari wana eneo Kimbiji ambapo wanatarajia kujenga chuo kitakachoendana na maono waliyonayo.Aidha amesema wanatarajia kuanzisha tawi Mikoa ya Lindi, Mwanza na kwamba wako katika mchakato wa kupata eneo Pemba kwa ajili ya kufungua tawi.

Mmoja wa wahitimu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Meli na Bandari kutoka Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar, Rajabu Ally Rajabu, amesema sekta ya bahari ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kwa sababu kwa zaidi ya asilimia 90 usafirishaji unafanyika kwa njia ya maji.

"Bahari inafanya kazi kubwa zaidi katika kusafirisha mizigo na bidhaa kwahiyo nitoe wito kwa vijana kujiunga na Chuo cha Bahari ili kunufaika na kozi mbalimbali ambazo zinatolewa...soko kubwa lipo ndani na nje ya nchi," amesema Rajabu.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Joseph Abdallah Meza, amekipongeza chuo hicho kwa kuandaa rasilimali watu mahiri katika sekta ya bahari na kuwataka wahitimu kutumia vema elimu waliyopata katika kukuza sekta hiyo.

Kongamano hilo lililenga kujadili chuo kilipotoka, kilipo na kinakotarajia kufika huku pia likiangazia namna bora ya kuwekeza kimkakati katika sekta hiyo.











Powered by Blogger.