MANDONGA, DULLA MBABE KUPIMANA UBAVU MULEBA
Mabondia maarufu wa ngumi za kulipwa nchini, Karim Mandonga na Dulla Mbabe wanatarajia kupanda ulingoni kupimana ubavu Desemba 26,2024 (Boxing Day).
Pambano hilo lililopewa jina la 'Tagi la Mama Samia' litafanyika Uwanja wa Zimbihile, Muleba mkoani Kagera ambapo mabondia mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi watapanda ulingoni.
Wakizungumza na waandishi wa habari Desemba 5,2024 jijini Dar es Salaam mabondia hao wameahidi kuwapa raha mashabiki wa masumbwi Tanzania hasa Kanda ya Ziwa.
Mandonga atachapana na Said Mbelwa, huku Dulla Mbabe akizipiga na mkongwe Mada Maugo.
Mandonga amesema atampiga Mbelwa kuliko alivyompiga mara ya kwanza huku akitamba kuwa kutumia ngumi aliyoipa jina la Kiberenge.
"Mimi ndio Mandonga Mtu Kazi, Said Mbelwa akae akijua kipigo kinamhusu sisi ni jiko la shamba halichagui...mara ya kwanza alishindwa kumaliza raundi na safari hii hatoboi raundi mbili kwa hii ngumi kiberenge," amesema Mandonga.
Naye Dulla Mbabe amesema; "Tunakwenda kwenye vita, yule Maugo anajiita Mbunge wa Rorya sasa nimwambie tu mimi ni Mbunge mtarajiwa wa Kisarawe.
"Pamoja na kwamba tunakaa wote Chanika siangalii hilo, safari hii nitamkanda, mara ya kwanza alijipendekeza nikamvunja kiuno sasa tukutane tarehe 26 mtaona nitakachomfanya," ametamba Dulla Mbabe.
Mapambano hayo yataambatana na uzinduzi wa muonekano mpya wa kinywaji cha Smart Gin ambao ni wadhamini wa pambano hilo.
Akizungumzia sherehe za uzinduzi wa Smart Gin mpya iliyoboreshwa na kuwekwa kwenye kopo Mratibu wa Matukio na Balozi wa kinywaji hicho, Bakari Khatibu, amesema siku hiyo kutakuwa na matukio mbalimbali kuhakikisha wale wote watakaofika wanafurahi.
"Safari hii tumekuja na muonekano mwingine mpya, katika kusherehekea uzinduzi huu tunaanza na tamasha la ngumi la kihistoria pale Muleba mkoani Kagera tukiwa pamoja na PeakTime ambao ni wadau wetu tupo nao kwa muda mrefu," amesema Khatibu.
