WANAFUNZI WATAKIWA KUWA WADADISI KWENYE MAFUNZO KWA VITENDO
Na Mwandishi Wetu, The Page
Wanafunzi wa vyuo nchini wametakiwa wanapokwenda kwenye kampuni mbalimbali kujifunza kwa vitendo wawe wadadisi na kuhoji maswali Ili waweze kuelewa kile wanachojifunza.
Hayo yamesemwa na Mhadhiri Msaidizi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Idara ya Ujenzi (DIT), David Hema, wakati wanafunzi wa chuo hicho walipotembelea ujenzi wa Mradi wa kituo cha Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kilichopo Feri Kivukoni kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo unaojengwa na Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC).
Hema amesema wanafunzi wanapokuwa wadadisi na kuhoji wanapotembelea kampuni husika kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo wataelewa kile walichojifunza kwenye vitabu
"Wanafunzi wetu wanapopita kwenye kampuni kama hii ya CCCC wanaweza kuonyesha uwezo wao wa kupata maarifa na nimefurahi kumuona mwanafunzi aliyesoma DIT amemaliza mwaka huu amechukuliwa na kampuni ya CCCC anafanya kazi hapa chini ya uangalizi," amesema Hema.
Amesema kampuni ya CCCC wanafanya miradi mikubwa sehemu mbalimbali ikiwemo nchini na nje ya nchi hivyo wanafunzi wanapoenda wanajifunza vitu vingi.
Naye Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Uhandisi Ujenzi wa DIT, Alvin Rujweka, amesema wamewapeleka wanafunzi wa Uhandisi wa chuo hicho Ili wajifunze kwa vitendo baada ya kufundishwa darasani kwa nadharia.
Rujweka amesema elimu inaelekeza zaidi kwenye kufundishwa kwa vitendo kwa kuwa wanafunzi hao wanaandaliwa kuwa wahandisi.
"Wanafunzi wakipewa elimu ya kwenye vitabu wanapomaliza wanapelekwa kwenye ujenzi unaendelea chuoni wanaunda kampuni wanashindanishwa itakayoshinda inapewa fedha na vitendea kazi wanaijenga kitu husika kwa mwaka huo wa masomo,"amesema Rujweka.
Rujweka amesema wanafunzi hao wakimaliza zoezi hilo wanapelekwa kwenye maeneo ambayo ujenzi wake unaendelea unafanywa na kampuni husika kwa wakati huo lengo wajifunze kwa vitendo
Mhandisi Msaidizi wa sehemu ya ujenzi huo, Benson Mbilinzi, amesema amepata uzoefu wa kuunganisha ujuzi wa darasani pamoja na unaofanywa na kampuni ya CCCC Ili aweze kuwa na ujuzi zaidi.
"Nawaomba wanafunzi wenzangu wajitokeze katika nafasi kama hizi mfano mimi nilikuja kupata mafunzo kwa vitendo tukaambiwa tuandike barua kwa atakayetaka kazi lakini wengi hawakuomba mimi niliomba na sasa nafanya kazi chini ya uangalizi wa kampuni ya CCCC," amesema
Kwa upande wake Meneja Usalama Tawi la Tanzania, kutoka Kampuni CCCC, Li Yuling amesema mradi wa BRT unatoa mchango mkubwa katika uchumi, maendeleo na uboreshaji wa maisha.
Amesema mradi huo ni sehemu muhimu ya urafiki wa China na Tanzania na kampuni ya CCCC inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya miundombinu pamoja na kuleta uchumi.
"Mradi unajumuisha ujenzi wa vituo muhimu vya usafiri, vituo vya mabasi na vifaa vingine vya trafik unalenga kuboresha ufanisi wa usafiri wa mijini, kupunguza msongamano na kuimarisha hali ya usafiri ya wakazi wa eneo hilo," amesema Yuling.
"Ili kuendeleza mafanikio hayo na kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, kampuni ya ujenzi ya China tawi la Tanzania imekutana na waandishi wa habari, kuzungumzia mafanikio hayo," amesema.
