CHALAMILA AWATAKA WANANCHI KUSHEREHEKEA KRISIMASI, MWAKA MPYA WAKIDUMISHA AMANI
Na Nora Damian, The Page
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wananchi kusherehekea Sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya kwa kuendelea kushikamana na kudumisha amani na utulivu.
Akizungumza leo Desemba 23,2024 amesema wamejipanga kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani na kusisitiza kuzaliwa kwa Yesu Kristo iwe ni kielelezo cha kudumisha upendo watu wasifanye maovu yatakayosababisha uvunjifu wa amani.
Aidha amewataka wazazi na walezi kuwalinda watoto wao na kujilinda wenyewe na kamwe wasifanye starehe kupitiliza wahalifu wakapata nafasi.
"Mheshimiwa Rais amesisitiza umuhimu wa kulinda amani katika mkoa wetu wa Dar es Salaam, wananchi washerehekee wakijua tuni ya amani ni jambo muhimu sana ambayo inapaswa isiharibiwe," amesema Chalamila.
Chalamila amesisitiza wananchi kutembea na vitambulisho wakati wote ili wanapopata majanga iwe rahisi kutambulika.
Mkuu huyo wa mkoa pia amezungumzia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP 11) na kusema utaanza kutekelezwa Januari mwakani na kuwataka wananchi kuendelea kulipa kodi ili kusaidia utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya Serikali.
Katika hatua ngingine amesema kuanzia Januari 2025 biashara katika jiji hilo zitafanyika kwa saa 24 na wataanza na Soko la Kariakoo huku wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wakiendelea kuainisha maeneo mbalimbali.
Mkuu huyo wa mkoa amevishukuru vyombo vya habari kwa kazi kubwa waliyofanya kwa mwaka wa 2024 na kuomba ushirikiano huo uendelee kwa mwaka 2025.

