SERIKALI KUUNDA BODI YA WATAALAM WA UCHUKUZI
Na Nora Damian, The Page
Serikali ipo katika hatua za kuandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Bodi ya Usajili wa wataalam wa uchukuzi ili kuhakikisha kazi zote za usafirishaji zinasimamiwa na watu wenye taaluma stahiki.
Hayo yamesemwa leo Desemba 20,2024 na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile wakati wa mahafali ya 40 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Amesema bodi hiyo itakuwa ikiwatambua, kuwasajili na kusimamia weledi na maadili ya wataalam wa uchukuzi Tanzania Bara.
Aidha amesema wanafarijika kuona idadi ya wahitimu katika maeneo ya kimkakati kama vile usafiri wa reli, usafiri wa maji na usafiri wa anga inaongezeka.
"Idadi hii ya wahitimu ni ushahidi tosha wa juhudi kubwa za chuo kuhakikisha tunakuwa na wataalam wa kutosha katika sekta ya uchukuzi. Natoa wito kwa uongozi wa chuo kuendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ili kukifanya chuo kuendelea kuwa mahali sahihi kwa kuandaa wataalam katika sekta hii," amesema Kihenzile.
Amesema pia Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya uchukuzi na kwamba uwekezaji huo unahitaji wataalam watakaoendesha na kusimamia kwa ustadi miradi husika kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi.
Ametaja baadhi ya uwekezaji huo ni ujenzi wa barabara na madaraja, reli ya kisasa, ukarabati wa meli, ujenzi na upanuzi wa bandari, viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege.
Naibu Waziri huyo amesema kwa kutambua umuhimu wa wataalam wa kutosha katika sekta ya uchukuzi Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo ya urubani, injini kwa ajili ya mafunzo ya uhandisi wa ndege pamoja na wahudumu wa ndani ya ndege.
Aidha amesema Serikali ilitoa ardhi hekta 60 eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya mafunzo ya taaluma za uaafiri wa anga.
"Jitihada hizi za Serikali zinafanyika ili kukiwezesha chuo kutoa elimu bora na kuandaa wataalam wa kutosha katioa sekta ya uchukuzi na usafirishaji. Serikali itaendelea kukiwezesha chuo ili kuhakikisha kinatimiza majukumu yake ya kuandaa wataalam, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam katika sekta ya uchukuzi kwa maendeleo ya taifa letu," amesema.
Amekiagiza chuo hicho kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati ili ianze kutumika kwa kuwa mahitaji ni makubwa sambamba na kutumia mapato ya ndani katika kuendeleza na kuboresha miundombinu ya chuo.
"Mfanye bidii kuhakikisha wahitimu wetu wanaendelea kuwa na moyo wa uzalendo kwa taifa, muongeze nguvu na kuwekez kwenye tafiti hususani kwenye eneo la uchukuzi ambalo ndiyo lengo la kuanzishwa kwa chuo hiki," amesema.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Dk. Prosper Mgaya, amesema kwa sasa chuo wanatekeleza Mpango Mkakati wa Nne wa miaka mitano (2021/2022) hadi (2025/2026) ambao umezingatia mahitaji ya sekta ya uchukuzi kwa lengo la kuhakikisha inapata wataalam wenye ujuzi na weledi watakaoweza kukabiliana na changamoto za maendeleo katika njia zote za usafirishaji kwenye sekta hiyo.
Aidha amesema kwa miaka mitano idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa asilimia 39.3 kutoka 10,988 mwaka 2020/2021 hadi 18,078 mwaka 2024/2025.
Amesema ongezeko hilo limetokana na mahitaji ya wataalam wa sekta ya uchukuzi lakini kutokana na jitihada za Serikali kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kililazimika kuanzisha kozi mpya zitakazokidhi mahitaji ya wataalam katika maeneo hayo.
Amesema pia ili kuongeza uwezo wa kitaaluma wa watumishi chuo kimeendelea kuwapeleka masomoni watumishi ma hadi kufikia mwaka 2024/2025 watumishi 72 wapo masomoni.
Amesema kati yao 45 ni wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Shahada ya Uzamili 23, wawili mafunzo ya urubani ambao wapo katika ngazi ya leseni za kurusha ndege za biashara, wawili leseni ya matengenezo ya ndege Ethiopia, saba wamemaliza leseni ya matengenezo ya ndege Ethiopia na Marekani na kufaulu, wanne wamepata leseni na watatu wanasubiri leseni zao.
