LATRA CCC WATAKA WATOA HUDUMA KUZINGATIA MATAKWA YA LESENI ZAO

Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini
LATRA CCC, Daudi Daudi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usafiri wakati wa Sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya.

Na Nora Damian, The Page

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) limewataka watoa huduma kuzingatia matakwa ya leseni zao kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinalingana na madaraja yaliyochaguliwa na abiria.

Akizungumza Desemba 19,2024 Katibu Mtendaji wa LATRA CCC, Daudi Daudi, amesema mapumziko ya mwisho mwaka yamekuwa na uhitaji mkubwa wa usafiri na wakati mwingine kuzidi uwezo wa watoa huduma.

Amesema abiria watoe taarifa sahihi pale ambapo watapatiwa huduma ambazo hazikidhi viwango kulingana na tiketi walizokata.

"Mapumziko ya mwisho wa mwaka kwa miaka mingi yamekuwa yakiambatana na uhitaji mkubwa wa wasafiri kuelekea sehemu mbalimbali za nchi yetu, uhutaji wa huduma za usafiri huongezeka sana na wakati mwingine kuzidi uwezo wa watoa huduma waliozoeleka katika vipindi vingine vya mwaka.

"Watoa huduma wategemee ongezeko kubwa la abiria ambao wengi wao sio wale ambao wamekuwa wakiwahudumia, hivyo wawapatie ushirikiano," amesema Daudi. 

Aidha amewataka abiria kufanya maandalizi mapema kwa vyombo wanavyotegemea kusafiri navyo na kukata tiketi kwa njia ya mtandao kuepuka usumbufu wa wapigadebe au kulipa nauli zisizo rasmi.

Baraza hilo pia limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara yatokanayo na ajali zinazoepukika.




Powered by Blogger.