CAMFED LASAIDIA WATOTO 595,000 WA SEKONDARI, VYUO

Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano wa Shirika la Camfed Tanzania, Anna Sawaki, akizungumza katika mahojiano na waandishi habari kwenye mkutano wa nne wa kimataifa unaojadili kuhusu ubora wa elimu, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Shirika lisilokuwa la kiserikali la Camfed Tanzania limetoa ufadhili kwa watoto zaidi ya 595,000 tangu lilipoanza shughuli zake mwaka 2006.

Takwimu hizo zimetolewa leo Novemba 12,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano wa Shirika la Camfed Tanzania, Anna Sawaki, wakati akizungumza katika mahojiano na waandishi habari kwenye mkutano wa nne wa kimataifa unaojadili kuhusu ubora wa elimu.

Amesema shirika hilo linafanya kazi kuhakikisha mtoto wa Tanzania anapata elimu bora kama ambavyo sera na miongozo ya Serikali inaelekeza.

"Ili mtoto wa kike aweze kusoma kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili anahitaji pia uwezo na uelewa na kutengenezewa mazingira ya kujiamini aweze kuzishinda na kutimiza malengo yake.

"Tumekuwa tukishirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba watoto wa kike ambao wanatoka kwenye mazingira magumu, mazingira hatarishi tunawatafuta na kuwasaidia mahitaji mbalimbali," amesema Sawaki.

Amesema wamekuwa wakiwasaidia watoto mahitaji ya shule, fedha na mengine na kwamba kwa zaidi ya miaka 16 tangu waanze wamesaidia watoto wa sekondari 590,000 wakati kwa vyuo ngazi ya cheti na stashahada wamewafikia watoto 5006.

Mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka huu wanatarajia kutoa ufadhili kwa watoto 655.

"Katika mkutano huu sisi kama Camfed tunashiriki tukiwa wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania, tunashirikiana na mtandao kuweza kuangalia mifumo mbalimbali ya elimu na sera kuhakikisha kwamba inamjali mtoto bila kujali hali ya fedha, familia, ulemavu au eneo anakotoka," amesema.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amepongeza jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali wa elimu na kwamba wamedhamiria kuhakikisha ulinzi wa watoto wanapokuwa majumbani, shuleni na kwingineko unazingatiwa.

Mratibu wa Taifa wa TENMET, Martha Makala, amesema mkutano huo unaangazia kuwa na mifumo bora, imara na thabiti ya elimu itakayowezesha elimu iweze kutolewa zaidi ya darasani.

Mkutano huo ambao umehusisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka katika nchi 16 barani Afrika wakiwemo pia wanafunzi, walimu, vyuo vikuu na wizara zinazohusika na elimu una Kaulimbiu isemayo; 'Kukuza Mifumo ya Elimu Imara kwa Maendeleo Endelevu barani Afrika'. 


Powered by Blogger.