JIJI LA DAR LATENGA SH BILIONI 14 KUKOPESHA WAJASIRIAMALI
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga zaidi ya Sh bilioni 14 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kujikwamua kiuchumi.
Hatua hiyo inafuatia baada ta Serikali kurejesha utolewaji mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza Novemba 11,2024 wakati wa kongamano la wajasiriamali lililolenga kuwaelimisha na kuwahamasisha kuhusu mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema wanaamini mpango mpya wa sasa utaimarisha usalama wa fedha za Serikali na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa ufanisi.
"Tayari tumetoa elimu katika kata zote 36 na mitaa 159 ya halmashauri kama ambavyo Serikali inaelekeza kutoa elimu kwanza kabla ya kutoa mikopo ili kuleta tija iliyokusudiwa," amesema Mabelya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema wananchi wengi wana ari kubwa ya kujikomboa kiuchumi hivyo watasimamia maagizo yaliyotolewa na Serikali kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
Halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri 10 za mfano nchini ambapo mikopo hiyo sasa itatolewa kupitia benki kwa lengo la kulinda fedha za Serikali na kuhakikisha zinarejeshwa kwa wakati.
Aprili mwaka jana Serikali ilisitisha kutoa mikopo hiyo kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zimejitokeza kisha kutangaza kuirejesha tena Aprili mwaka huu ambapo fedha hizo sasa zitakopeshwa kupitia benki.
