WAANDISHI SIMAMIENI MISINGI YA HAKI, USAWA KWA WAGOMBEA WOTE - DK. MAGHEMBE
Na Nora Damian, The Page
Serikali imewataka waandishi wa habari kuandika habari zinazosimamia misingi ya haki na kujali usawa wa wagombea wote ili kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 13,2024 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk. Grace Maghembe, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari wa mtandaoni kuhusu Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Amesema taarifa zisipoeleweka zinaweza kuleta taharuki kwenye jamii hivyo zinapaswa zijikite kuwaunganisha Watanzania na kuongeza upendo na mshikamano.
"Tunatambua umuhimu wa vyombo vya habari vya mtandaoni katika kuelimisha umma, hatakiwi mtu yeyote kuachwa nyuma ndiyo maana Serikali tumeona twende na mabadiliko hayo na tunawajibika kuwajengea uwezo," amesema Dk. Maghembe.
Aidha amesema hakuna maendeleo bila kuwa na Serikali za Mitaa na kusisitiza uchaguzi huo ni muhimu kila mtu ashiriki.
Naye Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Tamisemi, Mihayo Kadete, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuendelea kutoa elimu ya mpigakura na kuviasa visome na kuzielewa kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili vishiriki kikamilifu na kutumia haki yao ya kuhabarisha na kupata habari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (Jumikita), Shabani Matwebe, amesema watatumia vema mafunzo waliyoyapata kuhabarisha umma na kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu.
Katika mafunzo hayo Tamisemi pia imewapatia washiriki hao Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuwarahishia katika majukumu yao wakati wa mchakato huo.
