WATAHINIWA 974,229 WAFAULU DARASA LA SABA
Na Nora Damian, The Page
Jumla ya watahiniwa 974,229 wamefaulu mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2024.
Akitangaza matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Said Mohamed, amesema kati ya watahiniwa waliofaulu wavulana ni 449,057 na wasichana ni 525,172.
Amesema ubora wa ufaulu kwa watahiniwa waliopata madaraja A na B umeimarika ambapo watahiniwa 431,689 wamepata madaraja A na B ikilinganishwa na mwaka 2023.
Aidha amesema katika masomo ya Hisabati, Sayansi na Teknolojia wavulana wamefaulu zaidi kuliko wasichana.
Amesema baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 61 ambapo kati yao 45 walibainika kufanya udanganyifu na 16 waliandika lugha ya matusi katika karatasi za kujibia.
Baraza hilo pia limezuia matokeo ya watahiniwa 418 ambao waliugua au kupata matatizo mbalimbali na kushindwa kufanya mtihani na wamepewa fursa ya kurudia mtihani huo mwakani.
