MIRADI MAALUMU YA UJENZI KUTENGWA KUKUZA UWEZO WA WAZAWA


Na Nora Damian, The Page

Serikali inatarajia kutenga miradi maalumu kwa ajili ya kukuza uwezo wa wazawa waweze kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi.

Takwimu zinaonyesha kati ya Januari 2013 hadi Juni 2023 miradi ya ujenzi iliyotekelezwa ni 36,839 yenye thamani ya Sh bilioni 61.6 huku wazawa wakitekeleza miradi 35,351 yenye thamani ya asilimia 40.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 29,2024 jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi, Dk. Matiko Mturi, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji miradi ya ujenzi wakati wa mkutano mkuu wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Amesema hivi sasa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wanaandaa mwongozo wa kutekeleza miradi ya kujenga uwezo wa wazawa.“Shida yetu siyo kutekeleza miradi, shida yetu ni kutekeleza miradi yenye thamani kubwa, mipango iliyopo ni kuboresha vigezo na masharti katika zabuni na miradi ya ujenzi. Tutatenga miradi maalumu kwa ajili ya kukuza uwezo wa wazawa…tunataka kwa miaka mitano tuwe tumepata watu 1,500 yaani kila mwaka watu 300,” amesema Dk. Mturi.

Ametaja baadhi ya sababu za ushiriki mdogo wa wazawa kuwa ni kuchelewa kwa malipo kwa wakandarasi na washauri elekezi, masharti magumu na riba kubwa ya upatikanaji wa mitaji wastani wa asilimia 18 ambayo inasababisha gharama kubwa ya mtaji.

Sababu zingine ni kutotengwa kwa miradi mingi kwa ajili ya kukuza uwezo wa makandarasi wazawa, makandarasi na washauri elekezi kutoa bei za chini isivyo kawaida katika zabuni, ubinafsi miongoni mwa makandarasi na washauri elekezi wazawa, mtazamo hasi kwa taasisi za manunuzi na Sera ya Ujenzi ya Taifa ya mwaka 2003 kupitwa na wakati.Akifungua mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema Serikali itaendelea kutoa hamasa kwa wataalam wa ndani na kuwataka kuchangamkia fursa za miradi inayoendelea kutekelezwa nchini.

Aidha amesema licha ya kuwa na wataalam na kampuni za ndani uwezo wa kufanya kazi kubwa ni changamoto hivyo kutoa mwanya kwa wataalam na kampuni za nje kutekekeza miradi mikubwa na kusababisha fedha za kigeni kwenda nje ya nchi.

“Wazawa wanaweza kufanya kazi lakini wakati mwingine sisi wenyewe ndio tunaokuwa wa kwanza kwenda kuwatafuta wageni badala ya kufikiria kuwatafuta wazawa wenzake na kuongeza nguvu ya pamoja…niwaombe na kuwasihi tuendelee kujenga umoja na mshikamano wetu kwa sababu dhamira ya Serikali ni kubwa,” amesema Mpogolo.Amewahamasisha wataalam hao kushiriki katika zabuni za ujenzi wa miradi mikubwa ili kujenga uwezo wa kitaaluma na kupunguza utegemezi wa wataalam kutoka nje ya nchi.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk. Ludigija Bulamile, amesema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa miradi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha ubora wa majengo na usalama wa raia na mali zao.

Aidha amesema mwaka 2005 walianzisha mpango wa mafunzo kwa vitendo ili kuwaimarisha wahitimu wa vyuo vikuu hatua iliyochangiwa na Serikali kufadhili mafunzo hayo.

Kwa mujibu wa Dk. Bulamile, bodi hiyo imesajili wahitimu wa vyuo vikuu ambapo wanahakikisha wanasajiliwa ndani ya miaka miwili baada ya kuhitimu masomo yao.



 


Powered by Blogger.