KAMUSI YA KISWAHILI KWA KIHISPANIA KUZINDULIWA CUBA

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika nchini Cuba.

Na Nora Damian, The Page

Serikali inatarajia kuzindua kamusi ya Kiswahili kwa Kihispania kwa lengo la kuzidi kukitangaza Kiswahili katika lugha mbalimbali za kimataifa.

Kamusi hiyo pamoja na kitabu cha misemo cha Kiswahili kwa Kihispania vitazinduliwa wakati wa kongamano la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika nchini Cuba kuanzia Novemba 7 hadi 10 mwaka huu.

Akizungumza leo Oktoba 30,2024 jijini Dar es Salaam Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, amesema kongamano hilo litashirikisha washiriki zaidi ya 600 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

"Kwa muda mrefu jitihada za kukuza Kiswahili nje ya Tanzania zilikuwa hazizai matunda, tulikazana kufundisha wageni Kiingereza kwenda Kiswahili. Watafiti wamefanya tafiti wamesema tunakosea kwa sababu nchi nyingine hawaongei Kiingereza."Kwa sasa tumekuja na mpango wa kufundisha Kiswahili kwa lugha yako, sasa tunafundisha Kiswahili kwa Kihispaniola, miaka mingine tutaongeza lugha nyingine kuhakikisha kwamba tunakisambaza Kiswahili," amesema Dk. Ndumbaro.

Aidha amesema katika kongamano hilo watazindua mfumo wa kufanya tafsiri nyaraka kutoka lugha mbalimbali kwenda Kiswahili unaotumia Akili Mnemba ambao umepewa jina la 'Kilimanjaro Kiswahili Services'.

Waziri huyo amesema pia katika kongamano hilo kutakuwa na warsha na semina mbalimbali, wasilisho la makala za kitaaluma na zisizo za kitaaluma, maonesho ya kazi za utamaduni na onesho la kanga.

"Kutakuwa na hafla ya usiku wa mswahili ambapo kutakuwa na vyakula vya asili ya mswahili, ngoma za asili, miziki ya Kitanzania, simulizi za mahusiano kati ya Wacuba na Waswahili," amesema.

Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, hotuba ya ufunguzi wa kongamano hilo itashereheshwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Cuba.




Powered by Blogger.