TARURA YATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA UJENZI DARAJA LA MAWE LEBENYA

Daraja la Lebenya lililojengwa kwa mawe.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Gairo Mkoa wa Morogoro, imetekeleza agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kujenga daraja la mawe la Lebenya linalounganisha Wilaya za Kilindi, Gairo na Kilosa mkoani Morogoro.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 45 limejengwa kutokana na fedha zilizobaki wakati wa ujenzi wa Daraja la Berega.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalumu), George Mkuchika, alipokagua hatua iliyofikia ambapo ujenzi umefikia asilimia 75.

Amesema Rais Samia ametoa fedha ili kurejesha mawasiliano kwa wananchi kwa kujenga upya madaraja yaliyoharibiwa na mvua zilizonyesha mwaka jana ambazo ziliathiri miundombinu ya barabara katika maeneo mengi nchini."Nimefurahi agizo la Rais Samia limetekelezwa, hapa mnajengewa daraja tena mawe tupu, daraja hili litakapokamilika litasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi," amesema.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Gairo, Mhandisi Simon Masala, amesema wametekeleza agizo la Rais ambapo Sh bilioni 1.3 zilizobaki kwenye ujenzi wa daraja la Berega zilielekezwa zitumike kuboresha barabara ya Berega - Kinyolisi - Makuyu kilomita 18, ujenzi wa daraja la mawe na maboksi kalavati ambapo unatarajiwa kukakamilika Mei 2025.

Amesema daraja hilo linagharimu Sh milioni 373 na litakapokamilika litanufaisha kata saba zenye wakazi 766,507 na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kwa wakazi wa Wilaya za Gairo, Kilosa na Kilindi."Barabara hii ni njia fupi kutoka Kilindi mkoani Tanga kwenda Morogoro ambapo ni kilomita 18 tu kufika njiapanda ya kwenda Morogoro badala ya kupitia njia ya Gairo ambayo ni kilomita 44, ikikamilika itakuza uchumi kwani wananchi watasafirisha mazao yao misimu yote," amesema Mhandisi Masala.

Mkazi wa Kijiji cha Italagwe - Gairo, John Semwenda, ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo kwani litakapokamilika watasafirisha mazao yao hasa mbaazi kwenda sokoni kwa urahisi.



Powered by Blogger.