NAIBU KATIBU MKUU UCHUKUZI AIPONGEZA TMA TAARIFA ZA UTABIRI
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za hali ya hewa nchini ikiwemo kuongeza usahihi wa utabiri.
Nduhiye ameyasema hayo Oktoba 30,2024 baada ya kutembelea ofisi za TMA Dar es Salaam kufahamu majukumu ya kiutendaji, changamoto na mikakati ya kuimarisha taasisi hiyo.
Amesema yeye ni mmoja wa wadau wanaofuatilia, kuzingatia na kutumia taarifa za hali ya hewa na kwamba TMA ya sasa imepiga hatua.
"Taarifa zenu ni nzuri, niwapongeze sana TMA, mimi ni mdau wa taarifa zenu na nimekuwa nikizifuatilia, kuzizingatia na kuzitumia, naweza kusema TMA ya sasa si kama ile za zamani," amesema Nduhiye.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a, ameeleza maono na mikakati ya kuimarisha huduma na kuongeza ushawishi wa mamlaka hiyo na Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa.
Amesisitiza azma ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mafunzo ya rada za hali ya hewa katika Afrika.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TMA Ofisi za Zanzibar, Masoud Faki, amemshukuru Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kuitembelea TMA ndani ya muda mfupi tangu alipoteuliwa na kuahidi kufanyia kazi maelekezo aliyoyatoa.
