TMA YATABIRI MVUA NYINGI FEBRUARI - APRILI 2025

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza utabiri wa mvua za msimu, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetangaza utabiri wa mvua za msimu na kusema mvua nyingi zinatarajiwa kunyesha katika kipindi cha Februari hadi Aprili mwakani.

Akitangaza utabiri huo leo Oktoba 31,2024 jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a, amesema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida, Dodoma, Kaskazini mwa Mkoa wa Lindi na Kaskazini mwa Mikoa ya Mbeya na Iringa.

Aidha amesema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika Mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Mkoa wa Lindi, Kusini mwa Mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.

"Shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama kawaida katika maeneo mengi katika mvua za msimu wa 2024/2025. Hata hivyo, vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani," amesema Dk. Chang'a.Kuhusu mvua za vuli amesema zimeanza katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Pwani ya Kaskazini kama ilivyotabiriwa.

Hata hivyo amesema maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yameendelea kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu.

Mamlaka hiyo imewashauri wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo kwa kuzingatia hali ya unyevu wa udongo pamoja na kutumia taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa wilaya husika.


Powered by Blogger.