TAKWIMU WALIOJIANDIKISHA SERIKALI ZA MITAA NI SAHIHI - NBS


Na Nora Damian, The Page

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu ni sahihi.

Ofisi hiyo imesema idadi hiyo haijavuka ile inayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Akizungumza leo Oktoba 28,2024 na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, amesema makadirio ya idadi ya watu 32,987,579 wenye umri wa kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni sahihi kama taarifa zilivyotolewa na Ofisi ya Rais - Tamisemi. "Idadi ya watu nchini kwa mwaka 2022 haiwezi kulingana na idadi ya watu kwa mwaka 2024 kwa kuwa hivi sasa tayari miaka miwili imeshapita tangu ilipofanyika Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022," amesema Dk. Chuwa.

Aidha amesema uandikishaji wa watu wengi zaidi ya matokeo ya sensa kwenye baadhi ya mikoa umechangiwa na kiwango cha uhamaji wa watu kutoka mikoa mingine kwa sababu Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ilihesabu watu kulingana na mahali walipolala usiku wa kuamkia siku ya sensa.

Amesema pia kwa mwaka 2024 idadi ya watu nchini inakadiriwa kuwa milioni 66,278,276 ambapo watu 3,785,036 waliokuwa na umri wa miaka 16, 17 na 18 kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 hivi sasa wana umri wa miaka 18, 19 na 20 wamekidhi kigezo cha kujiandikisha kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.




 


Powered by Blogger.