WANAHABARI WAHAMASISHWA KUSHIRIKI SAMIA KALAMU AWARDS
Na Nora Damian, The Page
Waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwasilisha kazi zao ili kushiriki katika tuzo za habari za maendeleo zijulikanazo kama 'Samia Kalamu Awards'.
Tuzo hizo ambazo zilizinduliwa rasmi Oktoba 13,2024 zinaandaliwa kwa ushirikiano wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA).
Akizungumza leo Oktoba 24,2024 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben, amesema awali tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ilikuwa Oktoba 26 lakini wameongeza muda hadi Oktoba 30,2024.
"Uamuzi wa kuongeza muda umechukuliwa ili kutoa nafasi kwa wale waliokutana na changamoto za kiufundi ikiwemo kushindwa kupandisha kazi mitandaoni kutokana na matatizo ya mtandao na changamoto nyingine.
"Hii ni fursa adhimu kwa vyombo vya habari, waandishi wa habari na maofisa habari kuonesha umahiri wao wa kuchakata habari na kuthaminiwa kwa michango yao katika taaluma ya uandishi," amesema Dk. Rose.
Amesema mpaka sasa wamepokea maombi 250 kutoka mikoa 23 ya Tanzania Bara na kusisitiza kuwa kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na ambazo hazijawahi kuwasilishwa kuwania tuzo nyingine na zinazofuata taratibu za haki miliki.
Tuzo hizo zinalenga kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa uandishi, utangazajo na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari vya asili na mitandaoni ili kuchochea uandishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo, uwajibikaji, mila na tamaduni pamoja na kujenga chapa na taswira ya nchi.
