MAWAZIRI MAMBO YA NJE WAPITISHA AJENDA ZA CHOGM
Na Mwandishi Maalumu, Apia Samoa
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola wamepitisha ajenda Kuu ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Ajenda hiyo ni Ustahimilivu katika kufikia malengo ya pamoja ya kimaendeleo ‘One Resilient Common Future’ pamoja na ajenda nyingine zitakazojadiliwa katika vikao vya wakuu wa nchi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, naye ameshiriki mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya, Fiamē Naomi Mataʻafa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Samoa.
Mkutano huo umeridhia ajenda za ustahimilivu wa mazingira, ustahimilivu wa uchumi, ustahimilivu wa watu katika jamii na ustahimilivu wa taasisi zinazolinda demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu kuwekwa mezani kwenye mkutano wa ngazi za juu.
Mbali na ajenda hizo, mawaziri pia wamepokea na kupitisha taarifa za Jukwaa la Wanawake, Jukwaa la Biashara na Jukwaa la Vijana yaliyokuwa yakiendelea kwa wiki hii.
Vipaumbele vya Tanzania katika Mkutano wa CHOGM ni pamoja na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kuwezesha vijana na wanawake kiuchumi, kukuza matumizi ya teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kwa nchi wanachama.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Madola unafanyika kuanzia Oktoba 25 hadi 26,2024, ambapo Waziri Kombo atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
