KILICHOSABABISHA WATUMISHI HOUSING KUSHINDA TUZO YA AFRIKA
Na Nora Damian, The Page
Juhudi zilizofanywa na taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) katika kuleta suluhisho la njia nafuu za malipo za nyumba ikiwemo malipo endelevu yanayolipwa kipindi cha ujenzi bila riba na utaratibu wa mpangaji mnunuzi vimetajwa kama sababu zilizosababisha kushinda tuzo ya Afrika.
WHI imetunukiwa tuzo ya heshima ya nyumba za gharama nafuu zaidi Afrika inayotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (AUHF) ambayo inatambuliwa na Umoja wa Afrika.
Akizungumza leo Oktoba 23,2024 na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa WHI, Dk. Fred Msemwa, amesema tuzo hiyo ilitolewa hivi karibuni wakati wa mkutano wa mwaka wa AUHF uliofanyika Zanzibar.
“Tumepokea kwa heshima kubwa tuzo hii, inaashiria mafanikio katika juhudi zetu tangu taasisi ilipoanzishwa miaka 10 iliyopita, tunaishukuru serikali ambayo ilianzisha taasisi hii, ofisi ya rais imeweka miongozo ya kuisimamia na kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” amesema Dk. Msemwa.
Aidha amesema nyumba za WHI zinauzwa kwa bei nafuu kati ya asilimia 10 hadi 30 ikilinganishwa na nyumba kama hizo kwenye soko huku bei ikianzia shilingi milioni 38 hatua iliyowezesha Watanzania wengi kufikia ndoto zao za kumiliki nyumba.
Amesema tuzo hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kuwawezesha wananchi wake kupata makazi nafuu.
Mkurugenzi huyo amesema pia ushindi wa tuzo hiyo umetokana katika kubuni na kutekeleza miradi ya nyumba yenye gharama nafuu zaidi na kuleta unafuu kwa wanunuzi ikiwalenga watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kulingana na mkurugenzi huyo, taasisi hiyo imeshauza nyumba zaidi ya 1,000 huku ikitarajia kujenga nyumba nyingine za gharama nafuu katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Singida, Pwani na Dodoma kwa ajili ya watumishi wa umma katika sekta za afya na elimu ili waweze kupata makazi bora.
Naye Ofisa Uhusiano wa WHI, Maryjane Makawia, amesema tuzo hizo zinatambua michango thabiti ya kuendeleza sekta ya makazi barani Afrika.
Amesema tathmini ilihusisha kuangalia kazi halisi iliyotekelezwa na WHI pamoja na mazungumzo na wanufaika wa miradi yake. 
