CCM YARIDHISHWA UANDIKISHAJI SERIKALI ZA MITAA
Na Mwandishi Wetu, The Page
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla amesema kujiandikisha kwa wingi kwa wananchi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kumechagizwa na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Amesema miradi ya zahanati, madarasa, vituo vya afya imetekelezwa kwenye vijiji na vitongoji hivyo, wananchi wameona kazi ya Dk. Samia Suluhu Hassan," amesema Makalla.
Akizungumza leo Oktoba 22,2024 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amewapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano katika zoezi hilo.
Aidha amesema endapo chama hicho kitapoteza kwenye baadhi ya vitongoji, vijiji au mitaa wataheshimu matokeo na kwamba huo utakuwa wakati muafaka kwao kujitafakari na kujipanga kwa nini walipoteza ili iwe njia ya kufanya vizuri kwenye uchaguzi ujao.
Amesisitiza kuwa CCM haihitaji mbeleko kwani kwa takwimu walizopokea ndani ya chama na zile za Tamisemi na kwa maandalizi yaliyofanyika wanatarajia ushindi wa kishindo.
