TAMASHA LA 43 BAGAMOYO KUITANGAZA NCHI KIMATAIFA
Na Mwandishi Wetu, The Page
Wafanyabiashara na wajasiriamali wa sanaa za ufundi wanatarajiwa kunufaika na Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni ambalo linatarajiwa kufanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani kuanzia Oktoba 23 hadi 26, 2024.
Akizungumza na waandishi wa Habari Bagamoyo mkoani Pwani, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema lengo la tamasha halitakuwa ni kuitangaza Bagamoyo pekee bali nchi nzima na Afrika Mashariki.
Amesema wafanyabishara hao wataweza kuonesha na kuuza bidhaa zao kitaifa na kimataifa ikiwemo batiki, shanga magauni, hereni, vikapu ngoma, picha michoro, mashati, virutubisho na tibalishe.
Tamasha hilo ambalo litazinduliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, linalenga kuvutia wadau wa nje na ndani ya nchi ambapo pia litahusha shughuli za kisanii, kiutalii, kijamii na kiuchumi.
Amesema maandalizi ni mazuri na tayari kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali huku burudani zaidi zikitarajiwa kulinganisha matamasha mengine yaliyowahi kufanyika.
Amesema lengo la sasa ni kuhakikisha wanafikia tamasha la siku saba tofauti na ilivyo sasa la siku nne ili kusaidia vivutio vyote vya utalii vilivyopo Bagamoyo vinajulikana dunia nzima.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Sanaa Bagamoyo (TaSUBa), Dk. Herbert Makoye, amesema tamasha hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, makampuni binafsi, vyama vya siasa na viongozi wa dini mbalimbali.
Dk. Makoye amesema pia tamsha hilo litahusisha vikundi 74 ambapo 61 ni kutoka Tanzania Bara, 2 kutoka Zanzibar na 11 vya kimataifa kutoka Afrika Kusini, Zambia, India, Ujerumani, Brazili Hispania, Botswana, na Visiwa vya Mayotem (Ufaransa).
Vikundi hivyo vitafanya maonesho jukwaani ikiwemo ngoma za asili, muziki wa asili na wa kisasa, maigizo, sarakasi, vichekesho na mazingaombwe.
Tamasha hilo litatanguliwa na mkesha maalumu unaofanyika leo usiku.
