WANAOPATA MADHARA YA DAWA WATAKIWA KUWASILISHA MALALAMIKO TMDA

Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page
 
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) imesema inaendelea kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitenganishi na kuwataka wananchi wenye changamoto kutokana na matumizi ya dawa mbalimbali kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo.
 
Akizungumza Agosti 4,2024 na Waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma, Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa, amesema wamekuwa wakihakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini na zile zinazozalishwa katika viwanda vya ndani zimesajiliwa na mamlaka hiyo.

“TMDA inahakikisha bidhaa zinapimwa kujiridhisha kama zimekidhi vigezo na kuhakikisha zinazoingia kwenye soko zina ubora unaotakiwa, usalama na ufanisi. Ili tuweze kuhakikisha kuna usalama na ufanisi huwa kuna majukumu ambayo mamlaka inayafanya; bidhaa zote zinazoingia nchini zinasajiliwa na hata zile zinazozalishwa katika viwanda vyetu zinasajiliwa,” amesema Mkumbwa.
 
Aidha amesema TMDA inashiriki katika maonesho hayo kwa kutoa elimu kuhusu shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo ikiwemo udhibiti wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitenganishi pamoja na kupokea malalamiko na maoni kutoka kwa wananchi.
 
“Katika maonesho haya tunatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa, jinsi ya kupata huduma kama una malalamiko na tunayapokea na kuyafanyia kazi ili tuendelee kutoa huduma bora kwa Watanzania waweze kuwa na afya njema. Hivyo tunawakaribisha wananchi kutembelea banda letu na kuja kupata huduma mbalimbali,” amesema Mkumbwa.






 

Powered by Blogger.