TSB KUANZISHA VITUO VYA USINDIKAJI MKONGE KUWAINUA WAKULIMA WADOGO
Na Nora Damian, The Page
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) imesema ina mpango wa kuanzisha vituo vya usindikaji mkonge ili kumsaidia mkulima mdogo aweze kusindika na kupata singa (nyuzi) zinazokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.
Bodi hiyo inahamasisha kilimo cha zao hilo kwa sababu lina soko kubwa, linastahimili magonjwa, ukame na uhakika wa kipato.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mkuu Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka TSB, Simon Kibasa, amesema bodi imekuwa ikiwaunganisha wakulima ili wapate masoko na bei nzuri.
"Changamoto inayowakabili wakulima wadogo ni uhaba wa mashine za usindikaji hivyo, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tuna mpango wa kuanzisha vituo vya usindikaji kuwasaidia wakulima waweze kusindika na kupata singa zinazokubalika sokoni," amesema Kibasa.
Amesema bodi hiyo inahudumia wakulima wadogo, wakubwa na wa kati na kwamba wakulima wakubwa hawana changamoto kama ilivyo kwa wakulima wadogo.
Amesema wakulima wadogo wapo wanaolima kwenye mashamba yao binafsi na wanafanya biashara lakini wapo wanaolima kilimo cha mkataba kinachoendeshwa katika mashamba matano nchini yakiwamo Ngombezi na Magoma.
Amesema katika mashamba hayo yana mikataba kati ya mkulima mdogo na bodi ambapo inamkodisha mkulima kwa lengo la kulima na kutunza mkonge na kuna mkataba kati ya vyama vya ushirika vilivyopo katika mashamba hayo.
"Wote hawa wanasimamiwa na bodi kwa kushirikiana na ofisi ya msajili wa vyama vya ushirika Mkoa wa Tanga, katika maeneo hayo TSB imekuwa ikiwasimamia wakulima kuhakikisha wanapata bei nzuri kupitia wanunuzi mbalimbali," amesema Kibasa.


