DCEA: WAKULIMA LIMENI MAZAO MBADALA, BANGI INAHARIBU UOTO WA ASILI
Ofisa Elimu kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Said Madadi, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Na Nora Damian, The Page
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema licha ya madhara ya kiafya yasababishwayo na matumizi ya bangi na mirungi, kilimo hicho pia kinaondoa uoto wa asili.
Akizungumza Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Ofisa Elimu kutoka DCEA, Said Madadi, amesema sehemu zinazolimwa bangi na mirungi miti au mazao mengine hayalimwi na kuwa na hatari ya njaa baadaye.
Amesema maeneo ambayo yanalimwa bangi na mirungi hakuna miti mikubwa ambayo inatumika kutunza mazingira kwa kuhifadhi maji na upatikanaji wa hewa safi na mvua.
"Wanapolima bangi au mirungi wanakata miti mikubwa na sehemu kubwa wanazolima ni milimani ambapo kufikika ni vigumu, lakini ndipo ambapo uoto wa asili unatakiwa uwepo kwa ajili ya kulinda mazingira, kwahiyo tunawashauri wakulima kuacha kulima bangi na mirungi," amesema Madadi.

Mfamasia Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Upendo Chenya, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Amesema katika maonesho hayo wanatoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na wakulima kuacha kujihusisha na kilimo cha bangi na mirungi.
Kulingana na ofisa huyo, athari kubwa za matumizi ya mirungi ni kusababisha saratani na upungufu wa nguvu za kiume.
"Bangi inasababisha matatizo ya afya ya akili na katika moja ya dawa za kulevya ambazo zina kemikali nyingi kuliko dawa yoyote ni bangi...ina kemikali zaidi ya 400," amesema.
Naye Mfamasia Mwandamizi kutoka DCEA, Upendo Chenya, amesema ili kupunguza madhara wanatoa tiba kwa watumiaji au warahibu wa dawa za kulevya ambapo serikali imekuwa ikiboresha huduma za tiba hiyo katika vituo vya afya.
Amesema kuna vituo zaidi ya 16 ambavyo vimeweza kusajili zaidi ya watu 17,000 wanaopata huduma hiyo inayotolewa bure ikilenga kumsaidia mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida.
