DMI YAWAITA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UBAHARIA


Na Nora Damian, The Page


Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimewahamasisha wahitimu wa kidato cha sita na wale wenye stashahada kuchangamkia fani ya ubaharia kwa kuwa ina fursa nyingi zinazoweza kuleta manufaa ya kiuchumi na kuongeza ajira kwa vijana.

Chuo hicho ambacho kipo chini ya Wizara ya Uchukuzi kina jukumu la kutoa elimu na mafunzo kwa upande wa bahari, kutoa ushauri elekezi kwa taasisi za umma na serikali pamoja na kufanya tafiti zinazohusiana na sekta ya bahari.

Akizungumza Agosti 4,2024 katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji ( Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Msimamizi katika Kitengo cha Usajili wa Wanafunzi DMI, Bernard Mgendwa, amesema wanafunzi waliosoma masomo ya sanaa na sayansi wanaweza kusoma katika chuo hicho kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamili.
"Katika maonesho haya ya Nanenane tunatoa huduma ya kusajili wanafunzi wanaoomba kujiunga na chuo pia tunatoa ushauri kwa kozi mbalimbali na kuwaelekeza ufaulu unaotakiwa.

"Kwa wale wanaotaka kusoma ngazi ya shahada kwa upande wa sayansi tunatoa taaluma ya uhandisi na unahodha na oparesheni kwa upande wa bandari hii ni kwa waliosoma masomo ya sanaa," amesema Mgendwa.

Msimamizi huyo amesema usajili unaendelea hadi Agosti 10 mwaka huu na kwamba kutakuwepo na awamu ya pili ambayo itaanza Septemba 3 na kufungwa Septemba 21 na ngazi ya cheti awamu ya pili usajili umeanza Agosti 5, mwaka huu.

Amesema mwitikio wa wananchi katika maonesho hayo ni mkubwa kwani wamepata wageni wa rika mbalimbali ambao wamepewa mafunzo na kwamba wengi walikuwa hawafahamu kama kuna uhusiano wa shughuli zinazofanywa na chuo hicho na kilimo.

Amesema pia wanatekeleza dhana ya Uchumi wa Buluu kwa kuwapa wavuvi mafunzo ya usalama baharini na usalama kwenye maji.
Mgendwa amesema pia katika maonesho hayo wanatoa elimu sahihi ya vifaa vya uokozi, namna ya kujiokoa mtu anapopata shida kwenye maeneo ya bahari na ya maziwa makuu. 
Powered by Blogger.