TAEC YASEMA MIONZI INA FAIDA, WAKULIMA WASIIOGOPE
Na Nora Damian, The Page
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imesema mionzi ina faida nyingi kwa maendeleo ya ustawi katika jamii na kuwataka wakulima wasiiogope.
Akizungunza Agosti 03,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mtaalam wa Mionzi kutoka TAEC, Alphonce Mgina, amesema mionzi inatumika kwenye sekta mbalimbali kama afya, kilimo, mifugo na viwanda.
Amesema mionzi kwenye kilimo inatumika kuhifadhi chakula ili kiweze kukaa kwa muda mrefu na kuua baadhi ya wadudu ambao ni wasumbufu.
"Kwenye maonesho haya TAEC imekuja kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuweza kupambana na mionzi kwa kuwa ina faida katika maisha ya binadamu, ila ikitumiwa visivyo huwa inaleta madhara.
"Taasisi inajipambanua kuwasaidia wananchi ili waweze kupata huduma za mionzi kama wanaenda hospitali waweze kupata huduma za mionzi inayofaa," amesema Mgina.
Amesema pia wameweka vituo katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka kwa ajili ya kukagua vyakula vinavyoingia kama vimechafuliwa na mionzi.
"Tunaangalia vyakula vinavyosafirishwa kutoka ndani kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kulinda soko la Tanzania.
"Tumeweka watumishi wengi kwa lengo la kupambana na hili endapo kuna tatizo la mionzi tume inakuwa ya kwanza kupambana na tatizo hili," amesema.
Amesema katika maonesho hayo mwitikio wa watu kutembelea banda la TAEC ni mkubwa kwa kuwa wanatamani kujifunza kuhusu mionzi kwa kuwa wengine ni wasafirishaji wa vyakula.
Amewataka wananchi wa Dodoma na maeneo mengine kutembelea banda la TAEC ili waweze kujifunza faida za mionzi na hasara pale itakapotumika vibaya.
Amewataka wananchi wa Dodoma na maeneo mengine kutembelea banda la TAEC ili waweze kujifunza faida za mionzi na hasara pale itakapotumika vibaya.

