WANANCHI WAKOSHWA HUDUMA ZA BRELA IKISAJILI KAMPUNI 50 MAONESHO YA NANENANE


Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma wakipata huduma katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni.

Na Nora Damian, The Page

Baadhi ya wakazi wa Dodoma na maeneo mengine jirani wamejitokeza kupatiwa huduma mbalimbali katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini humo na kupongeza ubunifu wa wakala huo katika utoaji huduma.

Katika maonesho hayo BRELA inatoa huduma za usajili wa majina ya biashara, kampuni, alama za biashara, hataza kutoa leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kusajili viwanda vidogo na kulinda vumbuzi za wataalam mbalimbali.

Wakizungumza Agosti 6,2024 baada ya kutembelea banda la wakala huo kwenye maonesho hayo wananchi hao wamesema kuwepo kwa huduma hizo kumewarahishia kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara.
Mmoja wa wananchi hao Yahaya Hassan amesema; “Nilikuja kufuatilia taarifa za kampuni nashukuru nimehudumiwa vizuri na nimezipata kwa haraka, kama nisingekuja kwenye maonesho pengine ingenilazimu kuchukua siku tatu au zaidi.

Hassan amewashauri wananchi wengine wenye changamoto za kibiashara au majina ya kampuni kufika katika banda la BRELA kwenye maonesho hayo ili kupatiwa huduma kwa haraka.

Mkazi mwingine wa Nkuhungu, Juliana Obedi, amesema amefurahishwa na namna wakala huo ulivyojipanga kuwahudumia kutokana na timu ya wataalam iliyopo.

“Brela wanafanya vizuri maana ukija hapa wataalam wote wapo kwahiyo, lazima changamoto yako itatatuliwa. Tunaposikia maonesho kama haya tusiyapuuzie kuna huduma nyingi zinatolewa,” amesema Juliana.
Ofisa Kumbukumbu kutoka BRELA, Faridi Hoza, amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo hadi sasa wamesajili zaidi ya kampuni 50 na kuwataka wakulima na wafannyabiashara kutembelea banda lao kupata elimu na huduma mbalimbali.

“Ukija hapa kama una changamoto yoyote tunakuhudumia, tunahudumia wakulima, wafanyabiashara ili waweze kufanya maombi ya usajili na tunafanya usajili wa papo kwa papo kwahiyo, kama una changamoto au kuna sehemu ulikwama ukija hapa tunakusaidia,” amesema Hoza.

Powered by Blogger.