TARURA WAJIVUNIA MAABARA YA KUPIMA UDONGO UJENZI WA BARABARA

Fundi Sanifu Mkuu katika Maabara ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Jacob Manguye, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), umesema barabara wanazojenga zina viwango vinavyohitajika kwa sababu wanapima udongo kabla ya kuanza ujenzi.

Akizungumza Agosti 5,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Fundi Sanifu Mkuu Maabara ya Tarura, Jacob Manguye,
amesema ili barabara itengenezwe vizuri lazima ianze maabara kwa kupima sampuli za udongo, kokoto au lami.

Amesema barabara nyingi zinashindwa kuwa za kiwango kwa sababu ya kutopima udongo kabla ya kuanza ujenzi.

"Tarura tuna maabara ya kupima udongo ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kusimamia ubora wa barabara za kutoka vijijini hadi na mijini ambazo zinateketezwa katika miradi mbalimbali hapa nchini.
"Kazi ya maabara ni kuthibitisha ubora na kupitia maabara ya udongo tunatarajia kuwa na kazi nzuri za viwango zinazotakiwa ili kuondokana na kashfa za kazi kuwa chini ya kiwango," amesema Manguye.

Amesema kwa sasa barabara za Tarura zina ubora wa viwango vinavyotakiwa na kwamba wanajitahidi kupanua zipitike vizuri hadi vijijini.

Amesema wameshiriki maonesho hayo kwa sababu wana uhusiano na wakulima na wafugaji kwa kuwa hutumia barabara zinazojengwa na Tarura kusafirisha mazao yao.


Powered by Blogger.