NIT WAJA NA TEKNOLOJIA MPYA YA KUSAMBAZA MBOLEA SHAMBANI

Mashine inayotumika kusambaza mbolea shambani iliyobuniwa na Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samwel Maembe.

Na Nora Damian, The Page

Wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) katika fani ya Uhandisi wa Mitambo wamebuni teknolojia ya usambazaji mbolea shambani kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwapunguzia gharama wakulima.

Teknolojia hiyo ambayo imekuwa kivutio kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, imebuniwa na Mwanafunzi wa mwaka wa nne, Samwel Maembe.

Akizungumza Agosti 5,2024 na Waandishi wa habari, Maembe amesema mashine hiyo inafanya kazi ya kusambaza mbolea shambani inaokoa muda na kumpunguzia gharama mkulima.

“Wakulima wengi wamekuwa wakitumia mikono kusambaza mbolea shambani hali inayowaweza kusababisha kupata athari za kiafya kutokana na kemikali mbalimbali zinazotumika, lakini pia wanaweza kupata uchovu kutokana na ukubwa wa shamba kwahiyo, mashine hii itawarahishia kusambaza mbolea kwa ustadi na kupunguza gharama.
“Mashine ina mfumo wa umeme jua na ina matairi ambapo mkulima atakuwa anaisukuma, ataamua kiwango gani cha mbolea kitumike, ina uwezo wa kusambaza katika shamba la ekari moja hadi tatu kutegemeana na ukubwa wa shamba…kama mteja ana shamba la ekari 10 tunaweza kuiboresha zaidi,” amesema Maembe.

Amewashauri wakulima kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwani yanawarahisishia kulima kilimo chenye tija na kuzalisha kwa wingi.

Mwanafunzi mwingine wa mwaka wa nne, Omary Chamlango, amebuni mashine mbili ambapo ya kwanza inafanya kazi ya kutoa mafuta na siagi ya karanga na nafaka yoyote inayoweza kusagwa.

Amesema mashine hiyo yenye uwezo wa kusaga karanga kilo 45 kwa saa inampunguzia mkulima gharama iwapo angetumia mashine mbili kufanya kazi moja.
Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Omary Chamlango, akionesha mashine aliyoibuni inayofanya kazi ya kutoa mafuta na siagi ya karanga.

"Niliangalia mashine nyingi ambazo wakulima wanatumia hasa wadogo zinafanya kazi moja, zinafanya kazi ya kutoa siagi au mafuta, lakini hii inafanya kazi mbili kwa wakati mmoja, anatumia karanga kutoa mafuta na siagi,” amesema Chamlango.

Mwanafunzi huyo amebuni mashine nyingine inayotumika kuchanganya chakula cha mifugo yenye uwezo wa kuchanganya kilo 100 kwa saa.

“Mashine ina uwezo wa kukoboa nafaka ambazo ziko kwenye mfumo wa mbegu, mahindi, mchele au ngano. Utakuta mkulima anatumia mashine kukoboa, anatumia mashine kusaga lakini tukiwa na mashine moja ambayo inafanya kazi nyingi kwa wakati mmoja inamsaidia kuokoa muda na kumpunguzia gharama,” amesema.

Ofisa Uhusiano Mkuu wa NIT, Tulizo Chusi, amesema wanatumia maonesho hayo kuonesha bunifu hizo na kutoa elimu kwa umma kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.





Powered by Blogger.