WAKULIMA MILIONI SABA KUSAJILIWA MBOLEA YA RUZUKU 2025


Na Nora Damian, The Page


Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) imesema hadi kufikia mwaka 2025 idadi ya wakulima watakaokuwa wamejisajili kupata mbolea ya ruzuku itafikia milioni saba kutoka milioni nne za sasa.

Akizungumza Agosti 7,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma, Mwenyekiti Kamati ya Ruzuku ya Mbolea Taifa, Luis Kasera, amesema ili mkulima apate mbolea ya ruzuku ni lazima awe amejisajili na kuwasihi ambao bado kujitokeza na kujiandikisha.

Amesema ambao walisajiliwa kipindi cha nyuma watachukuliwa alama za vidole, picha zao na alama za mashamba yao kwa lengo la kujua alipo na shamba lake ili kurahisisha usambazaji wa mbolea hizo.
Mwenyekiti Kamati ya Ruzuku ya Mbolea Taifa, Luis Kasera, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

“Tunamshukuru sana Rais Samia baada ya kuona mbolea inazidi kupanda bei kutokana na Vita ya Ukraine na changamoto ya Covid aliamua kuweka rukuzu mwaka 2022/2023 na tutaendelea kutoa mpaka mwaka 2025/2026. Hii yote ni kwa ajili ya kumsaidia mkulima apate mbolea kwa bei rahisi na imfikie alipo ili aweze kuongeza tija kwa kupata mazao mengi ya chakula na kuuza.

“Tunawasihi wakulima wajitokeze kwa wingi kujisajili na watoe taarifa ambazo ni sahihi ili tuwasaidie na kuwafikia pale walipo,” amesema Kasera.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mbolea iliyopo kwa sasa ni zaidi ya tani 300,000 ambayo ni ya kupandia na kukuzia na kwamba malengo ni kufikia tani milioni moja na kuwataka wakulima wanunue mapema kwa sababu ipo ya kutosha.

“Bado kuna meli ambazo ziko njiani, tunategema msimu utakapoanza tutakuwa na zaidi ya asilimia 50 na itakapofika Desemba tutakuwa tumeingiza mbolea zote. Pia tuna viwanda viwili vinavyozalisha mbolea; Intercom wanatakiwa kufikisha tani 600,000 na Minjingu tani 250,000 lengo ni kuondoa utegemezi tukifika 2030 tuwe tunajitosheleza,” amesema.

Amesema pia wamesaini makubaliano na kampuni kutoka Indonesia kwa ajili ya kutengeneza mbolea ya Nitrojen ambayo inatumika kwa wingi na ni malighafi kwa viwanda vya ndani.
Mwenyekiti huyo amesema wamefungua maabara na ofisi katika mikoa kuhakikisha mbolea zote zinazoingia zina viwango na mkulima anapata ambayo ni sahihi.







Powered by Blogger.