GCLA YAWAFUNDA WAKULIMA, WAFUGAJI NJIA BORA KUSAFIRISHA MAZAO NJE YA NCHI

Meneja Kanda ya Kati wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Gerald Mollel, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page
 
Wakulima na wafugaji wametakiwa kuitumia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ili kujua njia bora za kusafirisha mazao nje ya nchi na kuweza kukubalika.
 
Mamlaka hiyo kazi zake kubwa ni uchunguzi wa sampuli na vielelezo mbalimbali ambapo inasimamia sheria tatu; Sheria ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Namba 8 ya mwaka 2016, Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya mwaka 2003 na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Vinasaba vya Binadamu Namba 8 ya mwaka 2009.
 
Akizungumza Agosti 7,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma, Meneja Kanda ya Kati wa GCLA, Gerald Mollel, amesema mamlaka hiyo huchunguza sampuli za jinai, mazingira, ubora wa vyakula na kutoa vyeti vya uchunguzi hasa kwa bidhaa zinazopelekwa nje ya nchi kwa biashara.
“Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ina ithibati ya ubora na inapochunguza sampuli zozote na kutoa majibu ya mazao au bidhaa nyingine lazima zitapokelewa nje ya nchi.

"Tunafanya uchunguzi mbalimbali, maziwa au mazao kama mahindi tunaangalia sumu kuhakikisha yanafaa kwa matumizi, asali tunapima na kutoa cheti cha hati ya uchunguzi kama inasafirishwa nje ya nchi kwahiyo tunawakaribisha wakulima waje wapate elimu kuhusu shughuli mbalimbali tunazozifanya,” amesema Mollel.
 
Meneja huyo amesema pia wanasajili wadau wanaoingiza kemikali za viwandani na majumbani ili kujiridhisha zina ubora kwa matumizi ya nchi na kwamba wana kanzidata kuhakikisha zinazoingia ni zile zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria.
 
Aidha amesema kemikali zinazopita kwenda nchi jirani wanasimamia kuhakikisha hazichepushwi na kwenda kutumika kutengenezea madawa mengine ambayo hayahitajiki.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira GCLA, Dk. Shimu Peter, amesema mamlaka hiyo ina kituo cha kuratibu matukio ya sumu ambapo imekuwa ikishirikiana na watoa huduma wa afya kunusuru maisha ya watu waliodhurika.
Kaimu Mkurugenzi Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira katika
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Dk. Shimu Peter, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

Kuhusu teknolojia ya vinasaba amesema inatumika katika uchunguzi wa jinai wa vinasaba, uhalali wa watoto, utambuzi wa binadamu wakati wa majanga, utambuzi wa viungo vya binadamu, utambuzi wa jinsi kwa wale wenye jinsia tata.
 
“Unapofahamu uhalisia wa watoto kwa wazazi inakusaidia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mirathi na inasaidia katika taasisi zingine ambazo zinaweza zikawa zinahitaji, teknolojia hii inatumika kupima vinasaba vya binadamu kufahamu kama kuna changamoto yoyote ya kiafya mfano watu wanaohitaji kupandikizwa figo.
 
“Watu wenye changamoto ya jinsia tata, watu ambao si waaminifu kama wabakaji lazima apime ili kujiridhisha mtuhumiwa halisi ambaye amefanya tukio, teknolojia inatumika pia kwenye majanga makubwa mfano miili ambayo imeharibika vibaya ili iweze kutambuliwa na ndugu,” amesema Dk. Peter.










Powered by Blogger.