WAKULIMA WAGAWIWA BURE MBEGU ZA ASILI WAENDELEZE ZISIPOTEE

Mbegu za asili za mazao mbalimbali zinazotolewa kwa wakulima kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page

Wakulima katika Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine ya nchi wamegawiwa bure mbegu za asili za mazao mbalimbali ili waziendeleze zisipotee.

Mbegu hizo zimetolewa na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) kwa wakulima hao kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoedelea kitaifa jijini Dodoma.  

Akizungumza Agosti 7,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhifadhi wa Bioanuai ya Mimea TPHPA, Dk. Neduvoto Mollel, amesema athari ambayo taifa linaweza kukumbana nalo iwapo mbegu za asili zitapotea ni kuwa tegemezi kwa mbegu zinazoingizwa kutoka kwa watu wengine.

Amesema tayari wameanzisha benki za jamii katika maeneo ya Karatu na Kusini mwa Tanzania ambapo wanawafundisha wakulima namna ya kutunza mbegu. 

Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhifadhi wa Bioanuai ya Mimea TPHPA, Dk. Neduvoto Mollel, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

“Mbegu za asili ni zile zilizokuwa zinatumika zamani na wakulima na babu zetu lakini sasa hivi hazitumiki sana, kwahiyo sampuli zake zinatunzwa kwa matumizi endelevu ya sasa na baadaye, zinaweza kutumika kurahisisha utafiti wa mbegu kwa lengo la kuboresha za sasa.

“Kama nchi ni lazima iwe na hifadhi ya kutunza mbegu ‘mama’ ili likitokea lolote tuwe na mahali pa kuanzia, hizi tulizonazo tumezitoa kwa wakulima kwa sababu bado wapo wanaotunza, tumetoa kwao lakini tunahamasisha waje wazichukue na kuziotesha…ubora wake tofauti na mbegu za sasa.

“Tunawahamasisha wakulima wahakikishe mbegu za asili hazipotei, yeyote mwenye mbegu ya asili au anayependa kuendeleza mbegu ya asili aje achukue sampuli na kutumia. Mbegu za asili zina Ladha tofauti mfano mchele wa zamani una ladha nzuri kulinganisha na mbegu ambazo zimeshabadilishwa,” amesema Dk. Mollel.

Amesema mbegu wanazohifadhi ni pamoja na za mazao ya mahindi, mpunga, maharage, mchicha, maboga, alizeti, dengu na nyingine na kwamba wakulima wengi waliopita katika banda lao wamechukua sampuli za mbegu za mahindi na maboga kwa lengo la kupata ladha ya zamani. 

Amesema mbali ya kuwa na benki ya mbegu kitengo kingine kilichopo ni cha hifadhi ya sampuli kavu za mimea na taarifa zake ambazo zinahifadhiwa kwa rejea ya baadaye na uhifadhi wa misitu ili kujua iliyo katika hatari ya kupotea.




Powered by Blogger.