SAGCOT YAJIVUNIA USHIRIKIANO WA MAREKANI KATIKA KUENDELEZA WAKULIMA NCHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page

Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga amesema ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Marekani katika kuendeleza wakulima nchini umeleta mafanikio makubwa.

Mpango huo unahudumia mazao 12 yakiwamo ya mbogamboga, soya, viazi, nyanya na chai.

Alikuwa akizungumza mara baada ya Balozi wa Marekani nchini, Dk. Michael Battle, kutembelea banda la wafanyabiashara wa parachichi kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

"Sehemu kubwa ya mafanikio yaliyopatikana Nyanda za juu Kusini si uzalishaji bali pia katika miundombinu mfano Barabara ya Morogoro ambayo inaenda kwenye Mto Kilombero maarufu kwa uzalishaji wa sukari na miwa.

"Kwa sasa tumeanza kuuza korosho katika Soko la Marekani na Balozi Dk. Battle amewahamasisha wafanyabiashara wanaoongeza thamani mazao na mafuta ya parachichi kuongeza juhudi," amesema Kirenga.
Kirenga amesema Balozi Dk. Battle alivyotembelea banda la maparachichi ameongea na sekta binafsi ambayo inauza matunda na inayoandaa utaratibu wa kupeleka nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Kirenga, Marekani ina kiu ya kupata matunda ya parachichi na mengine kutoka hapa nchini na Afrika na kwamba hiyo ni fursa ya kupeleka bidhaa katika soko la Marekani.

Balozi huyo wa Marekani ametembelea mabanda mbalimbali ya bidhaa, taasisi, makampuni na mashirika yanayofadhiliwa Serikali ya Marekani ambayo yameshiriki katika maonesho hayo na kuahidi kuendelea kufadhili shuguli za kilimo.

Vilevile kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mazao mbalimbali, kusafirisha bidhaa hizo na mazao ya Tanzania nchini Marekani sambamba na kufadhili shuguli zingine za uzalishaji maji na upatikanaji wa ajira.
Powered by Blogger.