KAMPENI YA MAMA SAMIA YAGUSA WENGI NANENANE


Na Nora Damian, The Page

Zaidi ya watu 387 wamepatiwa msaada wa kisheria kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia huku wengi wakiwa na matatizo ya mirathi na migogoro ya ardhi.

Kampeni hiyo ya miaka mitatu inayotekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ilianza Machi 2023 na inatarajiwa kukamilika Februari 2026. 

Akizungumza Agosti 6,2024 baada ya kutembelea maonesho hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Ealiakim Maswi, amesema tayari mikoa saba imefikiwa na mipango iliyopo ni kuifikia mingine 10 kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Ealiakim Maswi, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.

“Tangu tulipoanza maonesho tumeona watu 387 na kati yao 195 ni wanawake na 192 ni wanaume, tunatoa huduma ya usaidizi kwa Watanzania, tunasimamia na kusaidia upande wa mirathi, matatizo ya ardhi ambayo katika nchi yetu ni makubwa na mengine. Mama ametoa nafasi tutoe huduma ya msaada wa kisheria bila malipo kwa Watanzania.

“Tunapaswa tuisambaze katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar, mikoa mingine 10 kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tutapita kwa ajili ya kutoa usaidizi kwa Watanzania wenye matatizo…tunamshukuru sana Rais Samia kwa kukubali kusaidia Watanzania,” amesema Maswi. 

Mmoja wa wakazi wa Dodoma aliyefika katika banda hilo kupata huduma, Alexander Justine, amesema; “Nilikuwa sijui kama kuna huduma ya msaada wa kisheria kwenye maonesho haya, nilipofika hapa kwa kweli namshukuru Mungu nimepokelewa vizuri, wamenisikiliza na nimepata mwanga katika mgogoro wangu wa ardhi na jirani yangu. 


Powered by Blogger.