SHIRIKA LA DIANA LASAIDIA VYAKULA, MATIBABU KWA WATOTO WENYE ULEMAVU

Ofisa Maendeleo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwanaisha Ally (Wapili kulia), akimkabidhi pampasi Neema Ngowi, zilizotolewa na Shirika la Diana kusaidia watoto wenye ulemavu Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page
 
Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala mbalimbali ya kijamii (Diana Women Empowerment Organization) limetoa msaada wa vyakula na matibabu kwa watoto wenye ulemavu ambao wazazi na walezi wao hawana uwezo kukidhi mahitaji yao ya msingi.
 
Msaada huo unahusisha dawa kwa watoto watatu wenye ulemavu wa viungo na ambao pia wana kifafa na vyakula yaani unga, mchele, sukari, mafuta na sabuni kwa watu 50.

Akizungumza Agosti 28,2024 wakati wa kukabidhi msaada huo Ofisa Maendeleo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwanaisha Ally, amesema kuna mashirika 610 yaliyosajiliwa katika halmashauri hiyo lakini Shirika la Diana limekuwa na utararatibu wa kipekee kusaidia makundi ya wasiojiweza tangu walipoanza shughuli zao.
“Katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tuna mashirika 610, Shirika la Diana lina utaratibu ambao hauna ukomo tangu wameanza hadi leo wanatoa chakula na matibabu kwa watoto wenye changamoto za kiafya,” amesema Mwanaisha.
 
Mmoja wa wazazi Neema Ngowi, amesema ana mtoto wa kike mwenye miaka 25 ambaye ni mlemavu wa viungo na haongei na kwamba shirika hilo limekuwa likimsaidia vitu mbalimbali kama vile pampasi, taulo za kike na dawa za kifafa.

“Kwa muda mrefu Diana wamekuwa wakinisaidia, mwanangu ana changamoto ya kifafa akikosa dawa anaanguka, kama jana alikuwa hana dawa ameanguka usiku sikulala.
 
“Kila mwezi natakiwa kumpeleka Muhimbili kwenye kliniki yake na mimi naishi Mwanagati kwahiyo inanilazimu kupanda magari kwa kuunganisha hadi sita ili niweze kufika kwahiyo ni changamoto kwangu,” amesema Ngowi.

Mzazi mwingine Aziza Haziadi mwenye mtoto mlemavu wa viungo, amesema mwanawe ana miaka minane na ana changamoto ya kifafa ambayo wakati mwingine inasababisha kujing’ata mdomo lakini kupitia Shirika la Diana amekuwa akisaidiwa dawa zinazomwezesha kukua vizuri.

“Huu mdomo (anamuonyesha mwandishi) alijing’ata kikawa kidonda kikubwa, lakini sasa hivi kimepona. Tangu tuanze kupata dawa hasumbui tena na wala halii ovyo,” amesema Haziadi.
Mwenyekiti wa Shirika la Diana, Farida Kakhoo, amesema wamekuwa wakisaidia makundi mbalimbali ya kijamii kama vile wanawake, yatima, wenye ulemavu, wajane na wazee kwa kuwapatia vyakula, mavazi, huduma za kiafya na mafunzo ya ujasiriamali kuwawezesha kuondokana na changamoto walizonazo.
 
Kakhoo ameiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa bima ya afya ya watoto kwa sababu wazazi wengi wenye watoto wenye ulemavu hawana uwezo kukidhi mahitaji ya watoto wao huku wengine wakiwa wametelekezwa na waume zao.

Kwa mujibu wa Kakhoo, shirika hilo ambalo mwaka huu linatimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake lina matawi katika Mikoa ya Morogoro na Tanga limewezesha watoto zaidi ya 500 kupata elimu kuanzia msingi hadi elimu ya juu ambapo wengine wamefanikiwa kupata kazi maeneo mbalimbali na kuendesha maisha yao.

Powered by Blogger.