MOI YATAJA MBINU KUEPUKA MAUMIVU YA MGONGO
Dk. Consolata Shayo kutoka Kitengo cha Ubongo na Mishipa ya Fahamu Moi, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.
Na Nora Damian, The Page
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeeleza njia zinazosaidia kuepuka hatari ya kupata maumivu ya mgongo na kushauri wananchi kuzizingatia.
Akizungumza Agosti 6,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Dk. Consolata Shayo, kutoka Kitengo cha Ubongo na Mishipa ya Fahamu Moi, amesema tangu waanze kutoa huduma kwenye maonesho hayo wamebaini wananchi wengi wana matatizo ya mgongo, magoti na lishe duni.
Katika maonesho hayo wataalam hao wa Moi wameona wagonjwa wenye matatizo ya mifupa, ubongo, kichwa, mishipa ya fahamu, wenye matatizo ya lishe, wanaohitaji mazoezi tiba, viungo saidizi na huduma zote zinatolewa bure.
“Wengi wanaokuja ni wafanyakazi wa ofisini, unakuta mtu anakaa kwa saa tatu au nne hajasimama, hajanyosha mgongo au kutembea. Tunawashauri kutokaa zaidi ya dakika 45 mpaka saa moja bila kunyosha miguu na mgongo. Wengi wanakosa pia muda wa kufanya mazoezi tunawashauri kwa siku wajitahidi watembee angalau hatua 10,000, tupunguze kupanda lift, tupande ngazi.
“Usiku kabla ya kulala usile chakula kingi kwa sababu kama hupati muda wa mazoezi na kunyosha viungo lazima utapata matatizo ya mgongo,” amesema Dk. Shayo.
Daktari huyo amewashauri wananchi kubadili mtindo wa maisha na kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi ili kujiimarisha kiafya na kuepuka magonjwa mbalimbali.
“Kazi tunazozifanya tunakaa muda mrefu, tunakosa muda wa kufanya mazoezi, wengine wana lishe duni mifupa inachakaa kirahisi, tunawapa ushauri wa kibingwa na tunaamini wataimarika na kuendelea vizuri na shughuli zao…wale wanaohitaji kuonwa zaidi kwa ajili ya matibabu tunawaandikia rufaa na wengine tunawaandikia dawa,” amesema.
Amesema kuna mwitikio mkubwa wa watu waliotembelea banda lao kupata huduma mbalimbali na kuwasihi wengine wafike wafanyiwe vipimo kubaini matatizo yanayowakabili na kupatiwa tiba.
Amesema kuna mwitikio mkubwa wa watu waliotembelea banda lao kupata huduma mbalimbali na kuwasihi wengine wafike wafanyiwe vipimo kubaini matatizo yanayowakabili na kupatiwa tiba.



