FURAHIKA WAMUANGUKIA RAIS SAMIA VIFAA VYA KUFUNDISHIA
Mkurugenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Furahika, David Msuya, akizungumza wakati wa mahafali ya 19 ya chuo hicho, Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, The Page
Chuo cha Ufundi Stadi Furahika kilichopo Buguruni wilayani Ilala kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan awasaidie vifaa mbalimbali vya kufundishia kwa vitendo vitakavyorahisisha katika ufundishaji na kuwafanya wanafunzi waelewe masomo kirahisi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Chuo hicho, Dk. David Msuya, wakati wa mahafali ya 19 na kusema wanafunzi wakisaidiwa vifaa hivyo vitawasaidia kufundishwa kwa ufanisi masomo husika.
"Chuo chetu kinatoa elimu bila malipo wanafunzi wanachangia Sh 50,000 kwa ajili ya mitihani hivyo, rais wetu ni msikivu tunamuomba atusaidie vifaa mbalimbali vya kufundishia kwa vitendo ambavyo vitarahisisha katika ufundishaji.
"Wanafunzi 400 waliopita katika chuo hiki kati yao 230 wameajiriwa katika sekta za umma zikiwemo hoteli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar," amesema Dk. Msuya.
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Furahika kilichopo wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya chuo hicho.
Aidha amemshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira wezeshi kwa vijana ikiwemo utalii, uchukuzi ambapo vijana 31 wameajiriwa katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika kituo cha Mlandizi kilichopo mkoani Pwani.
Amesema chuo hicho kinatoa elimu ya ufundi kwa vijana wa kike na kiume ili kusaidia kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya na biashara ya kuuza miili kwa watoto wa kike.
Naye Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amewataka wahitimu wa chuo hicho kufanya kazi kwa bidii na kujiendeleza kitaaluma kwa kuwa elimu haina mwisho.
"Niwapongeze kwa kuhitimu mafunzo yenu katika fani mbalimbali jambo muhimu mnatakiwa mjiendeleze kitaaluma kwa kuwa kuna ushindani wa soko la ajira," amesema Zungu.
Amesema ajira zipo za kutosha endapo wahitimu wakijituma na kuwa wabunifu katika kukuza taaluma zao kwa kupitia ubunifu wao na wawe na nidhamu wanakokwenda watakuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho.
Zungu ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuunga mkono jitihada za rais kutoa elimu ya ufundi kwa vijana bila malipo na ameahidi kusaidia baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo.

