WANANCHI WATAKIWA KUKITUMIA KITUO CHA USULUHISHI MAHAKAMA KUU KUTATUA MIGOGORO

Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, akiwa katika banda la Kituo cha Ulusuhishi Mahakama Kuu kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Kituo cha Ulusuhishi Mahakama Kuu kimehimiza wananchi kutumia njia mbadala katika utatuzi wa migogoro ili kuokoa muda na gharama kulinganisha na ule unaotumika katika kesi za kawaida.

Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2015 kwa lengo la kurahisisha utatuzi wa mashauri ya madai yaliyofunguliwa kutoka Masjala za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Divisheni ya Ardhi.

Akizungumza Julai 8,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Rahel Kangagha, amesema mgogoro ukifika katika Kituo cha Usuluhishi unatakiwa uwe umekamilika ndani ya siku 30.
“Wateja wanapofungua kesi wanapobadilisha nyaraka zikikamilika hatua inayofuata ni ya usuluhishi, kwahiyo jaji anayesikiliza shauri anatoa amri kwamba limefika hatua ya usuluhishi. Wanaelekezwa wanakuja kituo cha usuluhishi, mchakato wa kusuluhisha unaanza,” amesema Hakimu Mkazi, Kangagha.

Hakimu Kangagha amesema wamefanikiwa kusuluhisha baadhi ya kesi na mashauri kuishia katika ngazi hiyo kisha kuandaa hati ya makubaliano na kurudisha shauri kwa jaji husika aliyekuwa akilisikiliza kwa ajili ya kulifunga.

Kwa mujibu wa Hakimu huyo, kwa kipindi cha Januari hadi Juni 30 mwaka huu kesi zilizopokelewa kwa ajili ya usuluhishi ni 150 na kati ya hizo 66 ni kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na 84 kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.

Amesema kati ya kesi hizo 38 zilifanikiwa kusuluhishwa na 97 zilishindikana na kurudishwa mahakamani kuendelea kusikilizwa.

“Hata kwa siku moja tunaweza kumaliza kesi iliyokuwa imeendeshwa kwa miaka miwili au mitatu, kuna faida za usuluhishi; kwanza unaokoa muda na kupunguza gharama. Unapokuwa na shauri mahakamani kwa ngazi ya mahakama kuu wengi wanataka kutumia wakili kitu ambacho ni gharama.

“Mchakato wa usikilizwaji wa mashauri kuna kuahirishwa hapa na pale, hivyo shauri linaweza kuchukua muda mrefu hata mwaka, lakini kwenye kituo cha usuluhishi mgogoro ukifika unatakiwa ndani ya siku 30 uwe umekamilika…matokeo yanaweza kuwa wakakubaliana, wakashindwana au wakakubaliana kwa sehemu,” amesema.

Amesema kituo hicho kinasaidia kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani, kudumisha mahusiano baina ya pande mbili zenye madai, kukuza uchumi kwa kuokoa muda na fedha ambazo mtu angetumia kufuatilia kesi husika.







Powered by Blogger.