TUMIENI MFUMO WA E - MREJESHO KUWASILISHA KERO SERIKALINI - KASWAGA

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Subira Kaswaga, akizungumza na waandishi wa habari katika banda la eGA kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam. 

Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imewataka wananchi kuutumia mfumo wa e - mrejesho kuwasiliana na serikali kwa kuwasilisha kero na changamoto mbalimbali ziweze kutatuliwa.

Kupitia mfumo huo ambao unapatikana kupitia simu za mkononi taasisi zote za umma zimeunganishwa hivyo mwananchi akiwa na kero anaweza kuwasiliana na Serikali ikazifanyia kazi.

Akizungumza Julai 12,2024 na waandishi wa habari katika banda la eGA kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa eGA, Subira Kaswaga, amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kujenga mifumo kurahisisha utendaji kazi katika utumishi wa umma.

Amesema umejengwa mfumo wa e - mrejesho ambao ni daraja la mawasiliano baina ya wananchi na Serikali.
"Kupitia mfumo wa e - mrejesho wananchi wanaweza kuelezea kero, changamoto, kutoa maoni au kuuliza swali lolote au hata kupongeza Serikali na yote yatafanyiwa kazi," amesema Kaswaga.

Aidha amesema mfumo huo unapatikana kupitia simu ya mkononi kwa kubonyeza *152*00# kisha namba 9 na kuendelea kufuata maelekezo.

Meneja huyo amesema taasisi zote za umma zimeunganishwa katika mfumo huo hivyo mwananchi akiwa na kero mbalimbali anaweza kuwasiliana na Serikali ikazifanyia kazi.

Kwa mujibu wa Kaswaga huduma hiyo inapatikana kwa kupakua app ya e - mrejesho au kwa kutumia tovuti ya www.emrejesho.co.go.tz.

Mfumo huo umetambuliwa kimataifa kama jukwaa huru ambalo linawasaidia wananchi kuwasiliana na serikali na kushinda tuzo katika Umoja wa Mataifa ya ubunifu wa huduma za umma zilitolewa nchini Korea.

Kaswaga ametaja mfumo mwingine wa kubadilishana taarifa serikalini ambao unawezesha mifumo kusomana kwa lengo la kurahisisha na kuboresha uwajibikaji serikalini.

Mpaka sasa taasisi ambazo zimeunganishwa na mfumo huo ni 141 na kati ya hizo mifumo 109 inasomana na kubadilishana taarifa.
Powered by Blogger.