SERIKALI YAOMBWA KUWAFUNGULIA VIWANDA VIJANA WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU

Askofu wa Kanisa la Golani Christian lililopo Gogoni Kibamba, Dk. Leonard Ntibanyiba, akizungumza kwenye ibada iliyofanyika katika Kanisa la Jubilee International lililopo viwanja vya Fisi Manzese jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, The Page

Kikundi cha Sambaza Upendo Amani na Umoja kimeiomba Serikali iwasaidie vijana wanaoishi mazingira hatarishi kwa kuwafungulia viwanda vidogo ili waweze kuzalisha bidhaa mbalimbali pamoja na kuanzisha mashamba waweze kulima kilimo cha matunda.

Pia vijana hao wapatiwe mitaji na mafunzo ya ufundi waweze kuwa na ujunzii utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Askofu wa Kanisa la Eden Life, Mary Mudrikati, akizungumza Julai 27,2024 wakati wakitoa misaada mbalimbali kwa watu wanaoishi mazingira hatarishi katika Kanisa la Jubilee Internatonal liliopo Uwanja wa Fisi.

Mudrikati amesema Serikali isaidie vijana hao namna ya kuwawezesha kuishi maisha salama na si hatarishi kwa kuwafungulia viwanda vidogo waweze kuzalisaha biashara mbalimbali pamoja na kuanzisha mashamba ya pamoja ya kulima kilimo cha matunda.
Diwani wa Kata ya Hananasif Kinondoni, Wilfred Nyamwija, akimkabidhi suruali Amir Athuman.

"Vijana hawa wasaidiwe kupatiwa mafunzo ya ufundi ili wapate ujuzi utakaowawezesha kutengeneza bidhaa mbalimbali watakazoweza kuuza na kujikwamua kiuchumi.

"Tunaamini Serikali yetu ni sikivu itashughulikia jambo hili na kupata ufumbuzi, kikundi chetu kimelenga kuhamasisha upendo, amani na umoja kwa dini zote tunaamini ndiyo msingi mkubwa wa amani nchini," amesema.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Internation Pentecoste (IPHC), Fredy Mhaiki, amesema baadhi ya wachungaji wa makanisa ya Pentekoste wa Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na kikundi hicho wamekuwa wakiwakusanya watoto na vijana wanaoishi mazingira hatarishi na kuwapa huduma ya kiroho kwa kuwafundisha neno la Mungu.

"Tumekuwa tukikutana na vijana na watoto wanaoishi mazingira hatarishi tunawapa huduma ya kiroho waweze kutoka kwenye makundi mabaya ikiwemo waliojiingiza kwenye uchangudoa, unywaji pombe uliopitiliza na waliojiingiza kwenye uvutaji wa dawa za kulevya," amesema Mchungaji Mhaiki.

Naye Diwani wa Kata ya Hananasif Kinondoni, Wilfred Nyamwija, amesema amefurahishwa na kanisa hilo kuanzishwa kwenye viwanja vya Fisi kwa kuwa watu wanaoishi eneo hilo ni wa mazingira hatarishi.

"Inaonyesha kanisa hili jinsi linavyowasaidia watu wa hali ya chini wote mnajua sifa za uwanja huu na lipo katikati ya mji lakini mchungaji ameona aje hapa ili watu waweze kupewa huduma za kiroho," amesema Nyamwija.

Pia amesema ibada hiyo ilikuwa ikiwasaidia vijana wanaoishi mazingira hatarishi, wazee na wajane ambao wamepewa vitu mbalimbali zikiwemo nguo.
Powered by Blogger.