WADAIWA SUGU TBA KUKOSA UMEME, BASHUNGWA AAGIZA WATIMULIWE

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akizungumza wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya nyumba zilizojengwa na Wakala wa Majengo (TBA) eneo la Magomeni Kota, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page
 
Wakati Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakianza kuweka mifumo ya kisasa itakayowanyima huduma za umeme na maji wapangaji ambao hawajalipa kodi, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza waondolewe kwenye nyumba bila kujali nyadhifa zao.

TBA imefunga mfumo wa kisasa wa ‘Payless’ ambao mpangaji akishindwa kulipa kodi ya pango atasitishiwa huduma ya umeme na maji mpaka atakapolipa.

Akizungumza Julai 23,2024 wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya nyumba zilizojengwa na TBA eneo la Magomeni Kota Dar es Salaam, Bashungwa amesema kuna uhitaji mkubwa wa kujenga makazi bora nchini wastani wa nyumba milioni tano huku mahitaji yakiongezeka kila mwaka.
“Kodi ya TBA ni theluthi mbili ya kodi ya soko, ukiona nyumba ya TBA haikufai uko huru kwenda kwenye nyumba nyingine zilizoko sokoni, fedha ambazo tunatumia kujenga nyumba za watumishi ni za Watanzania, wanaokaidi kulipa watoke wakapange mtaani nyumba ziko nyingi madalali wanawasubiri.

“TBA simamieni waondoke, wachukulieni hatua bila kuangalia sura zao au hadhi zao, wako watu wengi ambao wanasubiri mkitoka waingie,” amesema Bashungwa.
Aidha ameutaka wakala huo kushirikiana na sekta binafsi katika miradi mbalimbali waliyonayo kwa kuwa mikakati ya serikali ni kuitoa katika utegemezi wa ruzuku.
 
Kuhusu changamoto za miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam amesema tume inayoshirikisha Wakala wa Barabara (Tanroads), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na wizara iko mbioni kukamilisha kazi ya kutathmini njia za maji kwa lengo la kukabili adha ya mafuriko.

Akizungumzia vivuko vya Kigamboni amesema serikali iko mbioni kuleta kivuko kipya kitakachoendeshwa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na Wakala wa Ufundi (Temesa).
 
“Najua kuna changamoto ya vivuko, vimekuwa spana mkononi mara kwa mara vinatengenezwa, tutashirikiana na sekta binafsi ambayo italeta kivuko cha kisasa, tuko mbioni kufanya uzinduzi,” amesema.
 
Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro, amesema jengo lililozinduliwa ambalo lina nyumba 16 za watumishi limefungwa mfumo wa kisasa ambapo mpangaji akishindwa kulipa kodi atakosa huduma ya umeme na kwamba unaweza kutumika pia kusitisha huduma za maji na gesi.

“TBA itaendelea kuweka mfumo huu katika majengo yote yatakayokamilishwa hivi sasa, baada ya kuthibitika ubora wake utafungwa katika nyumba zetu zote nchini,” amesema Kondoro.

Amesema mradi huo umegharimu Sh bilioni 5.687 na kwamba wanaendelea na ujenzi wa jengo la tatu na la nne ambao umefikia asilimia 15.


Powered by Blogger.