MRAMBA AITAKA TPDC KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI USAMBAZAJI GESI ASILIA

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kushirikisha sekta binafsi ili kurahisisha usambazaji gesi asilia majumbani na kwenye magari.

Akizungumza Julai 9,2024 baada ya kutembelea banda la TPDC kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), amesema wanataka shirika hilo liwe na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi na eneo ambalo wanataka waongeze ushiriki wao ni katika gesi asilia.

“Tunataka gesi iliyopatikana nchini isambae kwa haraka zaidi, isambae kwenye vituo vya kujaza kwenye magari, isambae majumbani. Tunataka kuona sekta binafsi inashirikishwa zaidi katika usambazaji wa gesi majumbani na gesi za kwenye magari, kama tukiendelea kutegemea TPDC itachukua muda mrefu kuwafikia Watanzania wengi, lakini tukishirikisha sekta binafsi wakasambaza mabomba majumbani, kujenga vituo vingi vya CNG, wakaenda mpaka mikoni gesi hii itasambaa haraka,” amesema Mhandisi Mramba.Aidha amesema wanatarajia kuongeza vituo vya kujaza gesi kwenye magari kwa kuanzia katika Jiji la Dar es Salaam na hadi kufikia mwakani wanatarajia kuwa na vituo zaidi ya 30.

Amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu watakuwa wamejenga vituo Muhimbili, Kibaha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sinza, Mwenge, Goba, Mbezi Beach, Mbagala na kwamba baadhi vitajengwa na TPDC na vingine sekta binafsi.

“Hili la kuwa na kituo kimoja cha Ubungo Maziwa na Airport tutaachana nalo ndani ya mwaka huu na mwakani, tutakuwa na magari mengi yanazunguka ndani ya jiji wateja watafikiwa na kujaza gesi, kwahiyo suala la kujaza gesi kwenye magari tunajaribu kulirahisisha kwa kadiri inavyowezekana ili kuondoa adha kwa watumiaji.

Katibu Mkuu huyo pia ameitaka Kampuni tanzu ya shirika hilo (GASCO) kujitangaza zaidi kwani Watanzania wanahitaji huduma hasa katika ujenzi na usimamizi wa miundombinu.

Kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta amesema mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 30 na hadi sasa kilomita zaidi ya 600 za mabomba zimeshaingia nchini na wanatarajia utakamilika mwishoni mwa mwaka 2025.

“Mradi huu umezungumzwa muda mwingi, umeanza kuzungumzwa tangu awamu ya tano, awamu hii ya sita, ni mradi mkubwa unachukua muda mrefu, ujenzi unahusisha usanifu, kulipa watu fidia, kujenga mtambo mkubwa wa kufanya mafuta yasipoe lakini ujenzi unakwenda kwa kasi,” amesema Mramba.

  






Powered by Blogger.