WATUMIAJI GESI ASILIA KWENYE MAGARI WAFIKIA 5,000, EWURA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), James Andilile, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), James Andilile amesema kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia kwenye magari kumepunguza matumizi ya dola katika uagizaji nishati ya mafuta na kuwahamasisha wawekezaji kujitokeza katika ujenzi wa vituo. 

Akizungumza Julai 9,2024 katika banda la mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Andilile amesema kwa sasa magari 5,000 yamefungwa mfumo wa gesi asilia.

Andilile alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, kutembelea banda la mamlaka hiyo.“Matumizi ya dola yamepugua kwa sababu gesi tunayotumia katika magari inapatikana nchini, tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kusambaza gesi, nawaahidi tukipata maombi yao tutayashughulikia kwa haraka kwa sababu tunataka wananchi wapate huduma katika ubora unaotakiwa,” amesema Andilile.

Akizungumzia sekta ya mafuta amesema wanaendelea kuimarisha ubora na kufuatilia mwenendo wa bei katika soko la dunia na kwamba hadi kufikia Juni 30 ubora wa mafuta ulikuwa umefikia asilimia 97.

Katika sekta ya maji amesema wanahakikisha uwekezaji unaofanywa na serikali unawezesha kupatikana huduma endelevu na kwamba wanahakikisha ubora wa huduma unaimarika. 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameipongeza EWURA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za nishati.

Mhandisi Mramba amesema ubora wa huduma ya umeme umeimarika na kwa sasa hakuna changamoto ya kukatika kwa umeme kutokana na maboresho yanyoendelea kufanyika.

Aidha amesema wanahakikisha EWURA inafanya kazi zake kwa kufuata sera na sheria zilizopo katika mazingira yanayokubalika ndani ya sekta husika.




Powered by Blogger.