EWURA WAJIZATITI KULINDA MASILAHI YA MLAJI, MWEKEZAJI KWENYE SEKTA WANAZODHIBITI

Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), wakimsikiliza mteja kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba)  Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema inahakikisha inalinda masilahi ya mlaji na mwekezaji katika sekta inazodhibiti.

Akizungumza Julai 11,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo, amesema mamlaka hiyo ndio inayopanga bei za huduma zote na kwamba ni lazima zipeleke maombi mamlaka hiyo ifanye mchakato kwa kuangalia ubora wa huduma husika.

Kaguo pia amesisitiza mtu anapokwenda kujaza mafuta achukue stakabadhi ili kurahisisha ulipaji fidia pindi inapotokea ameharibikiwa na gari baada ya mafuta aliyojaza.

“Umekwenda kwenye kituo pengine umejaza mafuta gari ikakorofisha, tunawaambia Watanzania wawe wanachukua stakabadhi kila wanapojaza mafuta. Ukishakuwa nayo ndani ya siku saba elewana na mwenye kituo, sisi tutakwenda kupima mafuta na kama yalisababisha gari kuharibika itabidi mwenye kituo afidie gharama ya kukarabati gari na adhabu atapewa,” amesema Kaguo.

Amesisitiza kuwa kama mafuta yalikuwa na matatizo na kusababisha gari kuharibika mwenye kituo atapaswa amfidie gharama za ukarabati na adhabau atapewa.

Kuhusu maji amesema malalamiko makubwa ni kwenye ankara na kwamba walitoa miongozo kwamba ankara zote ziwe zinasomwa wakati mwenye dira yupo na si kushtukiza kama zamani.

“Sasa hivi hakuna cha kusema kwamba geti limefungwa, litafunguliwa mbele yako halafu unasoma, na baada ya kusoma utakuja ujumbe mfupi kwenye simu unaokuonyesha, ujumbe unakaa siku tatu kumfanya mtumiaji ahakiki kama hajabambikizwa. Na kama hajasema lolote inakuja ankara ya kulipia…haya ni maagizo ambayo tumeyafanya kuhakikisha Mtanzania anapata huduma anayostahili na ndiyo kazi ya mdhibiti,” amesema.

Meneja huyo amesema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara kujiridhisha namna ambavyo mamlaka inatibu maji na iwapo wateja wanaridhika na huduma.

“Tulitengeneza mfumo wa kushindanisha mamlaka, kuna mamlaka inayoongoza kitaifa na kuna mamlaka inayoongoza kwa kuwa mwishoni. Kwa kufanya hivyo ushindani ni mkubwa, kila mtu anapambana akifanyiwa tathmini awe bora, kwa kufanya hivyo naona huduma ziko tofauti na zinakuwa nzuri,” amesema Kaguo.
Amesema pia walitoa muda kwa mamlaka kuhakikisha zinakuwa na mfumo wa dira lakini akapendekeza kuwepo kwa dira za kulipa kabla.

“Kila mwaka EWURA huwa inatayarisha ripoti za mamlaka ya maji ambayo inaonyesha mamlaka ipi ni bora kuliko nyingine, inafanya uwajibikaji na uwazi uwe mkubwa. Kwenye maji tunapopanga bei tunashirikisha wadau wote na bei inayokuja inakuwa inaeleweka.

“Kwenye uwajibikaji watu wakipata huduma ambazo si bora wanalalamika, wakilalamika wasipoelewana EWURA inageuka kama mahakama, inaanza kuendesha kesi. Kama mamlaka ya maji ilitenda kosa atapata fidia, kama mteja ulitaka fidia na huipati tutakuambia tu,” amesema.

Kuhusu gesi asilia amesema wanadhibiti miundombinu ambapo masuala yanayoangaliwa zaidi ni mazingira, afya na usalama wa mali.

Amesema gesi imesaidia katika uzalishaji wa umeme nchini, inatumika kupikia katika baadhi ya taasisi, viwanda zaidi ya 50 Dar es Salaam na Pwani vinatumia.

Aidha amesema wanahamasisha watu wabadilishe mfumo na kuitumia gesi asilia iliyokandamizwa kwa sababu inaokoa gharama ambazo zingetumika kwenye mafuta.

“Matumizi ya CNG ni muhimu sana ndiyo maana tunahamasisha Watanzania wabadilishe magari, wenye uwezo wawekeze kwenye vituo vya mafuta kwa kuwa TBS alisharekebisha viwango vya vituo vya mafuta. Hadi sasa tuna vituo sita na magari yanayotumia gesi yamefika 5,000…tunahamasisha Watanzania waendelee ili tufike mahala tuwe na nishati mbadala.



Powered by Blogger.