TAFITI 187 KUWASILISHWA KONGAMANO LA KISAYANSI MUHAS

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Applolinary Kamuhabwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la 12 la kisayansi la chuo hicho. Kushoto ni Mkurugenzi wa Tafiti, Machapisho na Bunifu, Dk. Nahya Salim.

Na Nora Damian, The Page

Tafiti 187 zinatarajiwa kuwasilishwa katika kongamano la 12 la kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Kongamano hilo litakalofanyika Juni 27 na 28,2024 katika Kampasi ya Mloganzila litashirikisha wajumbe zaidi ya 400 kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo Juni 24,2024 na Waandishi wa habari Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Applolinary Kamuhabwa, amesema tafiti 80 zitawasilishwa kwa njia ya maongezi na 107 zitawasilishwa kwa njia mabango.

“Chuo kitaonyesha matokeo ya tafiti za hivi karibuni ya sayansi kutoka miradi mbalimbali ya tafiti zinazotoka ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miaka ya nyuma. Jamii ya wanataaluma wa MUHAS watapata fursa ya kushirikishana matokeo yao na kubadilishana mawazo na wataalamu pamoja na wadau kutoka sehemu mbalimbali za nchi na duniani kote.

“Lengo kuu ni kuboresha afya kupitia tafiti, chuo pia kitaeleza mafanikio ya tafiti na athari zake kwa upande wa kijamii na maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Amesema matokeo ya tafiti zitakazowasilishwa katika kongamano hilo ni kuhusu wagonjwa wenye Virusi vya UKIMWI (VVU) ambapo asilimia 15 wana kiwango cha juu cha sukari huku unywaji pombe na shinikizo la juu la damu vikitajwa kuchangia.

Tafiti zingine zitahusu upatikanaji wa huduma za wodi maalumu za kulaza watoto wachanga, utafiti uliofanyika Kinondoni ambao umebaini asilimia 54.5 ya wanawake wanatumia vipodozi vya kujichubua wangi wao ni wale wanaofanya mapokezi.

Vilevile mijadala itahusisha ufanisi wa kugharimia mifumo ya afya nchini ambapo watafiti watawasilisha jinsi nchi itakavyoweza kutekeleza mfumo huo kuleta tija kwa wananchi wote na mifumo bora ya kuishi kulingana na magonjwa yasiyoambukiza.

Profesa Kamuhabwa amesema tafiti hizo zimeainishwa katika mada ndogo ambazo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza, afya ya akili, upasuaji na lishe, magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea dhidi ya dawa, afya ya mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana rika, utunzaji na afya ya kinywa.

Mada nyingine ni viamuzi vya kijamii kwa afya, utafiti wa mifumo ya afya, tiba mbadala na asili, uvumbuzi wa dawa na maendeleo ya chanjo, masuala mtambuka; maadili na taaluma, akili bandia, teknolojia na afya ya kazini.

“Tumefanya tafiti zetu kulingana na mwenendo wa hali ya magonjwa duniani na Tanzania, sasa hivi duniani kote kuna mabadiliko ya magonjwa, kisukari, shinikizo la damu, saratani na mengine yanazidi kuongezeka. Kuna mlipuko wa Uviko 19 haya yote yanahitaji kutafutiwa majibu na yanapatikana kwa kufanya tafiti,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Kongamano la mwaka huu litatumika pia kumuenzi aliyekuwa mkuu wa chuo hicho Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi aliyefariki Februari 27,2024 ambapo katika miaka 17 alipokuwa mkuu wa chuo kilinufaika kwa mchango wake katika upanuaji wa miundombinu ya kufundishia, kutoa huduma na tafiti ikiwemo kampasi mpya ya Mloganzila.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ‘Sayansi kama hadithi ya maisha; nguvu ya tafiti bunifu na ushirikiano kwenye kuimarisha mifumo thabiti ya afya’ imechaguliwa mahususi kwa sababu mwelekeo wa magonjwa hapa nchini na duniani umekuwa ukibadilika mara kwa mara ambapo changamoto kubwa sasa ni kwenye magonjwa yasiyoambukiza.






Powered by Blogger.