MAHAKAMA YAJIVUNIA MABORESHO UENDESHAJI MASHAURI DHIDI YA UJANGILI
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, akizungumza wakati wa kikao kazi cha wadau wa haki jinai kujadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu, Dar es Salaam.
Na Nora Damian, The Page
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema maamuzi mbalimbali yanayotolewa dhidi ya mashauri yanayohusu ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu yameboreshwa ili kulinda rasilimali hizo na haki za binadamu.
Hatua hiyo inafuatia mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ushirikiano wa Taasisi inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori (PAMS Foundation) yaliyoshirikisha majaji wa mahakama kuu, mahakimu, waendesha mashitaka na wapelelezi wa ngazi mbalimbali.
Akizungumza leo Juni 19,2024 wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa haki jinai amesema mafunzo hayo yamesaidia kutekeleza sheria mbalimbali katika kulinda wanyamapori na misitu na haki za binadamu.
Kikao hicho kinachojadili changamoto zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili, uhifadhi wa wanyamapori na makosa ya misitu kimeshirikisha wadau wa haki jinai kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (OTM), Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kikosi cha Kupambana na Ujangili na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
"Maamuzi yameboreshwa zaidi baada ya kupata mafunzo kutokana na uelewa unaoheshimu uwepo wa utajiri mkubwa wa wanyamapori na misitu," amesema.
Aidha amewaelekeza watumishi wa mahakama kuisoma ripoti ya Tume ya Haki Jinai kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo yametajwa yanayogusa shughuli za kila siku za mahakama.
"Huu ni wakati wa sisi kuwa sehemu ya utekelezaji wa yale ambayo yametajwa katika tume hii. Tuwahimize watumishi na kuwasimamia wasome taarifa ya tume hii, isibaki kwa viongozi, ishuke kwa wananchi itusaidie kuboresha haki jinai, ulinzi wa wanyamapori na haki za wanyama," amesema Profesa Juma.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji Profesa Paul Kihwelu, amesema mafunzo wanayotoa yanalenga kutatua changamoto za sasa na baadaye.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Fortunata Msofe, amesema wanatarajia mafunzo hayo yataboresha uendeshaji wa mashauri dhidi ya ujangili na uhifadhi wa wanyamapori na kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kati ya mwaka 2022 na 2024 yalijumuisha washiriki 827 kutoka mikoa 26 na kufanyika katika vituo vya Morogoro, Katavi, Iringa, Tanga na Mara.
Washiriki ambao ni majaji wa mahakama kuu, mahakimu, waendesha mashitaka na wapelelezi wa ngazi mbalimbali wamejengewa uwezo kuboresha upokeaji wa taarifa za uhalifu wa makosa ya wanyamapori, ukamataji, upekuzi, uchukuaji na uhifadhi wa vielelezo, upelelezi, uendeshaji wa mashauri, usikilizaji, uandishi wa hukumu na utoaji adhabu.