MVUA YAUA WATU 50 TANZANIA

Wananchi wa Kijiji cha Muhoro wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye usafiri wa boti baada ya kukumbwa na mafuriko.

Na Nora Damian, The Page

Zaidi ya watu 50 wamefariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.

Vifo 28 zimeripotiwa kutokea katika halmashauri nane za Mkoa wa Morogoro, vifo 19 vimeripotiwa na jeshi la polisi katika Mikoa ya Lindi, Njombe, Tanga, Pwani, Morogoro, Manyara, Geita na Rukwa na vitano vimetokea katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Kisarawe mkoani Pwani.

Takwimu hizo zimetolewa leo Aprili 12,2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.

“Mafuriko yalitabiriwa na kutangazwa na athari zake haziepukiki, bado tunaendelea kukusanya taarifa katika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyokumbwa na mafuriko.

"Si kweli kwamba Bwawa la Nyerere limesababisha mafuriko bali limepunguza kwa kiasi kikubwa. Wingi wa maji haufikii maji yaliyokuwa yanapita mwaka 1974…kama kusingekuwa na bwawa mafuriko yangeanza kusumbua tangu Oktoba mwaka jana,” amesema Matinyi.


Amesema katika Mkoa wa Pwani mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa mazao mengi ya chakula, makazi na miundombinu ya barabara ambapo kata 12 zimeathiriwa na watu 1,014 wameokolewa.

Kwa mujibu wa Matinyi, katika Mkoa wa Morogoro nyumba 1,035 zimebomolewa, nyumba 6,874 zimezingirwa na maji, ekari 34,970 zimeharibiwa na mifugo 1,644 imeathiriwa.

Msemaji huyo amesema hatua ya kufungulia maji katika Bwawa la Nyerere ilichukuliwa kwa kuangalia vipimo vya kitaalam na kwamba halijasababisha mafuriko.

MIAKA 60 YA MUUNGANO

Sherehe za kitaifa za kuadhimisha miaka 60 ya Muungano zitafanyika Aprili 26 katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Matinyi amesema uzinduzi rasmi utafanyika Aprili 14 Zanzibar kisha utafuatiwa na maonesho ya kibiashara yanatakayofunguliwa Aprili 19 na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdulla, katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

Aidha kuanzia Aprili 15 hadi 31 kutakuwa na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchi nzima, Aprili 22 kutafanyika maombi katika wilaya zote nchini, Aprili 23 uzinduzi wa kitabu cha historia cha ofisi ya makamu wa rais na Aprili 25 tamasha la miaka 60 litakalofanyika nchi nzima.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano inasema ‘Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeshikamana na tumeimarika kwa maendeleo ya taifa letu’.





Powered by Blogger.