TANZANIA KUNUFAIKA ZIARA YA RAIS SAMIA UTURUKI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan anayotarajia kuifanya nchini Uturuki.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ametaja maeneo sita ambayo Tanzania itanufaika kutokana na ziara inayotarajiwa kufanywa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki.
Ziara hiyo ya kikazi ya siku tano inatarajiwa kuanza Aprili 17 hadi 21,2024 inatokana na mwaliko wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.
Mara ya mwisho Rais wa Tanzania alitembelea Uturuki miaka 14 iliyopita na Rais wa Uturuki alikuja nchini mara ya mwisho mwaka 2017.
Akizungumza leo Aprili 15,2024 na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Makamba amesema Tanzania itasaini mikataba na hati za makubaliano katika maeneo sita yakiwemo ya elimu ya juu hasa katika eneo la ufadhili wa masomo na masuala ya sayansi na teknolojia.
“Hii ni ziara ya kihistoria kwa sababu ni muda mrefu tangu Rais wa Tanzania atembelee Uturuki, hivyo ni ziara muhimu na ni heshima kubwa ambayo rais wetu amepewa.
“Uturuki ni nchi inayokua kwa kasi, ipo katika kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa na imeweka msisitizo wa kuimarisha mahusiano yake na Afrika, bidhaa nyingi tunanunua Uturuki na nyingi tunauza Uturuki…ni nchi ambayo tunataka tuwe nayo karibu,” amesema Makamba.
Amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kisiasa pamoja na kibiashara na kiuchumi kwa sababu Tanzania inahitaji mitaji, teknolojia na wawekezaji zaidi.
Kwa mujibu wa Makamba, Rais Samia atafanya mazungumzo rasmi ya kiserikali yatakayohusisha maeneo ambayo Tanzania inashirikiana na Uturuki pamoja na kuangalia mengine mapya.
Aidha atakwenda Mji Mkuu wa Biashara, Istanbul ambako kutafanyika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki.
Amesema Rais Samia atakutana na wawekezaji wakubwa 15 wa Uturuki kwa lengo la kuwashawishi kuja kuwekeza nchini.
Takwimu zinaonyesha kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kimeongezeka kutoka Dola milioni 9 miaka sita iliyopita hadi kufikia Dola milioni 22 mwaka 2023 ambapo Tanzania inauza zaidi bidhaa za mazao na madini.
“Uturuki wanauza zaidi kwetu lakini tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi ndio maana tunakwenda, tutaweka mfumo na utaratibu wa kubadilishana wataalam katika maeneo ambayo yana tija kwetu kama ya uzalishaji chakula, viwanda na sekta ya ujenzi,” amesema Makamba.