JENGO LA YANGA HALIBOMOLEWI
Na Nora Damian, The Page
Serikali imesema jengo la Klabu ya Yanga lililopo katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam halitabomolewa kwa kuwa halijaguswa na mradi wa upanuzi wa Bonde la Mto Msimbazi.
Akizungumza leo Aprili 12,2024 na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema mradi huo unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) utaanza kutekelezwa Aprili 15.
“Tathmini ilishafanyika na nyumba ambazo zinatakiwa kubomolewa zinajulikana zimewekewa alama, kazi ya ubomoaji itaanza hivi karibuni na itadumu kwa miezi mitatu…jengo la Klabu ya Yanga halimo hivyo halitabomolewa,” amesema Matinyi.
Kwa mujibu wa Matinyi, tayari Serikali imelipa fidia Sh bilioni 52.61 kwa wananchi 2,155 na sasa inakamilisha malipo kwa wananchi 446 ambao walikuwa bado hawajafanyiwa tathmini.
Mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano unagharimu Sh bilioni 675 pia utahusisha ujenzi wa miundombinu ya kukabiliana na mafuriko, daraja la jangwani na karakana ya mabasi yaendayo haraka.
